Hayo ni kwa mujibu wa Omar bin Abdullah bin Ali Al Bariki ambaye atawakilisha Oman katika Mashindano ya Tatu ya Kimataifa ya Qur'ani ya Wanachuo Waislamu ambayo yatafanyika Iran mwezi ujao wa Januari.
Akizungumza na IQNA, Ali Al Bariki ameongeza kuwa mashindano ya kimataifa ya Qur'ani yanasaidia kuimarisha ufahamu wa Qur'ani miongoni mwa washiriki.
Amesema kuwa anasubiri kwa hamu kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani nchini Iran na kusema: 'kwa kushiriki katika mashindano kama haya ya kimataifa, ninajitahidi kuimarisha uwezo wango wa tajwidi na Kiraa ya Qur'ani Tukufu'.
Ameongeza kuwa mashindano hayo ni fursa kwa washiriki kutoka nchi mbalimbali kujuana na kujifunza kuhusu utamaduni wa kila moja.
"Katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani, wawakilishi wa nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu hushindana katika kusoma na kuhifadhi Qur'ani Tukufu ambacho ni kitabu cha Waislamu wote. Jambo hili huimarisha umoja wa Kiislamu", amesisitiza Omar bin Abdullah bin Ali Al Bariki.
Akiashiria shughuli za Qur'ani nchini Oman, Al Bariki amesema mashindano kadhaa ya Qur'ani hufanyika nchini humo kila mwaka na kupokelewa kwa raghba na watu wote hasa vijana.
Al Bariki anasema alianza kujifunza Qur'ani akiwa bado mdogo kwa kutumia mbinu za kiraa zilizoidhinishwa na Chuo Kikuu cha Al Azhar. Ameongeza kuwa anaiga mbinu ya usomaji wa maustadhi kama vile Muhammad Seddiq Minshawi, Muhammad Mahmoud Tablawi na Mustafa Esmaeel.
Abdullah bin Ali Al Bariki ni mwanachuo wa fani ya teknolojia za kielimu katika Chuo Kikuu cha Sultan Qaboos mjini Masqat .
709983