IQNA

Mashindano ya Qurani ya watoto yaanza Yemen

8:43 - December 12, 2010
Habari ID: 2046180
Mashindano ya kitaifa ya tilawa na tajwid ya Qur'ani Tukufu kwa ajili ya watoto wa kati ya umri wa miaka 9-12 yameanza Disemba 11 katika mji mkuu wa Yemen, Sana'a.
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, mashindano hayo yanafanyika kwa himaya ya Kituo cha Kuhifadhi Qur'ani cha Wizara ya Waqfu na Masuala ya Kiislamu cha Yemen kwa ushirikiano na Kanali ya Televisheni ya Al Jazeera ya Watoto.
Abdulrahman al Muzalim Naibu Mkuu wa Kituo cha Kuhifadhi Qur'ani katika Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Yemen amesema kuwa: "Mashindano haya yatawashirikisha watoto 150 katika vitengo viwili vya watoto wa kiume na kike kutoka mikoa yote ya Yemen na yataendelea kwa muda wa siku tatu".
Ameongeza kuwa, watoto hao watashindana katika tilawa na tajwid ya Qur'ani Tukufu na baada ya hapo watano bora watashiriki katika fainali itakayofanyika nchini Qatar, makao makuu ya kanali ya satalaiti ya Al Jazeera.
Wakati huo huo Hamud Abdul-Hamid Al-Hitar Waziri wa Wakfu na Masuala ya Kiislamu wa Yemen amepongeza kanali ya Al Jazeera kwa kuandaa mashindano hayo na kuzingatia Qur'ani Tukufu na ukuzaji wa vipawa vya Qur'ani miongoni mwa watoto. Amesema kuna umuhimu wa kuhudumia na kueneza mafundisho ya Qur'ani Tukufu na Suna ya Mtume SAW.
710707
captcha