IQNA

Wakristo wa Basra kushiriki kwenye maombolezo ya siku ya Ashura

16:16 - December 14, 2010
Habari ID: 2047720
Kufuatia kuanza mwaka mpya wa Miladia sambamba na kuwadia mwezi wa Muharram, Wakristo wa Basra hawatafanya sherehe zozote za kukaribisha mwaka huo mpya bali wataungana na Waislamu katika kuomboleza kifo cha Imam Hussein (as) katika siku ya Ashura.
Akizungumzia suala hilo mbele ya waandishi habari, Sa'd Mata Botrous, Mkuu wa Kamati ya Wafuasi wa Dini za Waliowachache katika mji wa Basra amesema kuwa kwa kuzingatia kuanza mwaka mpya wa Miladia sambamba na mwezi wa Muharram na vilevile kwa sababu ya kukumbuka tukio la kulipuliwa kigaidi kanisa moja la Kikristo hivi karibuni mjini Baghdad, Wakristo wa mji huo wameamua kutofanya sherehe zozote za furaha za kukaribisha mwaka mpya. Amesema Wakristo wa mji huo katika mwezi wa Muharram watakuwa wakishiriki katika maombolezo yanayofanyika kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya Imam Hussein (as) na hasa katika siku ya Ashura.
Sa'd Mata Botrou amesema kwa mwaka wa pili mfululizo, Wakristo watakumbuka siku ya kuzaliwa Isa Masih (as) au kwa jina jingine Yesu Kristo kwa kushiriki katika ibada maalumu makanisani na kwamba wasomi wa Kikristo wamewausia wafuasi wao wasijihusishe na sherehe zozote za furaha na nderemo nje ya makanisa hayo.
Botrous ameongeza kuwa Wakristo wa Basra wameshirikiana na vijana wa Kiislamu wa mji huo kuanzisha makundi kadhaa ya maombolezo ya Imam Hussein (as), lengo likiwa ni kuimarisha umoja, ushirikiano na kushajiisha hisia za kuishi pamoja kwa amani wafuasi wa dini tofauti. 712152
captcha