Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Makarii na Mahafidhi wa Qur'ani wa Misri Sheikh Abuleinain Shueisha ambaye pia ni msomaji mashuhuri wa kimataifa wa Qur'ani. Ameongeza kuwa kuitisha mashindano ya Qur'ani ya kimataifa makhsusi kwa ajili ya wanafunzi Waislamu wa vyuo vikuu ni suna njema na hatua muhimu ya kustawisha na kupanua utamaduni wa Qur'ani katika nchi za Kiislamu na kueneza mafundisho ya kitabu hicho duniani. Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inastahiki kusimamia tukio hilo adhimu.
Akifafanua zaidi msomaji huyo mashuhuri wa Qur'ani amesema kuwa Iran daima imekuwa ikilipa kipaumbele suala la kuhifadhi na kuitisha mashindano ya kimataifa ya Qur'ani na hiyo ni suna na ada njema ambayo inapaswa kupongezwa. Sheikh Shueisha amesema, suala la kueneza mafundisho ya Qur'ani duniani hususan katika nchi zisizokuwa za Kiislamu ni matarajio ya kila Muislamu, na Mwenyezi Mungu akipenda Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatimiza matumaini hao ya Waislamu.
Katibu Mkuu wa Makarii na Mahafidhi wa Qur'ani amesema kuwa ameitembelea Iran mara kadhaa na kushangazwa na jinsi Qur'ani Tukufu inavyopewa umuhimu. Amesema kuwa aliona watoto wadogo wakisoma kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu kwa sauti nzuri na ya kuvutia ilhahi hawawezi kuzungumza hata sentensi moja ya Kiarabu. Sheikh Shueisha amesisitiza kuwa jambo hilo ni miongoni mwa miujiza ya Qur'ani. 712273