IQNA

Mifarakano huwaletea Waislamu adhabu

11:48 - December 22, 2010
Habari ID: 2051497
Ayatullah Ali Taskhiri, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kiamataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu amesisitiza kwamba kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'ani Tukufu mifarakano na udhaifu wa Waislamu huwaletea adhabu na kufri.
Ayatullah Taskhiri ameyasema hayo alipoonana na kuzungumza na ujumbe wa wanachuo wa Algeria na kusisitiza juu ya umuhimu wa kuimarishwa ukurubishwaji wa madhehebu ya Kiislamu kwa sababu ndiyo njia pekee ya kuleta umoja na mshikamano kati ya Waislamu. Amesema umoja huo unaweza kupatikana tu kupitia vitendo vizuri vya Waislamu. Ameendelea kusema kuwa tofauti za mitazamo ni jambo la kawaida kabisa na kwamba hakuna wakati ambapo fikra za binadamu zitakuwa sawa katika kila jambo lakini kwamba kadiri zinavyozidi kukaribiana ndivyo wanadamu wanavyozidi kukaribiana kimawazo na kivitendo.
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu amesema kwamba Waislamu wote wanaafikiana katika asilimia 90 ya misingi ya dini na kwamba tofauti ndogondogo zilizopo kati yao zinahusiana na matawi ya dini tu. Amesema kama Waislamu watajifunza namna ya kunufaika na hitilafu hizo kwa maslahi ya umma wa Kiislamu basi hitilafu hizo zitakuwa ni rehema, lakini iwapo zitatumika kwa lengo la kuugawa umma wa Kiislamu zitakuwa na madhara makubwa kwa jamii nzima ya Kiislamu.
Ayatullah Taskhiri ambaye pia ni mshauri wa Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kiutamaduni ameashiria mashambulio ya kigaidi yaliyotekelezwa hivi karibuni huko Chabahar kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa maadui wa mfumo wa Kiislamu wa Iran wanafanya juhudi kubwa za kuzusha fitina na mgawanyiko wa kimadhehebu katika taifa la Iran kupitia vitendo vya kigaidi lakini kwamba Wairani wanatambua vyema kwamba ndugu zao Wasuni hawahusiki na vitendo hivyo bali ni vibaraka wachache sana miongoni mwao ndio wanaotumiwa na vyombo vya ujasusi vya Marekani na Uingereza kuvuruga usalama wa Iran.
Ujumbe huo wa Algeria umemshukuru sana Taskhiri kutokana na juhudi zake za muda mrefu za kuimarisha ushirikiano na umoja miongoni mwa Waislamu wa madhehebu tofauti katika ulimwengu wa Kiislamu. 716161
captcha