IQNA

Mashindano ya Mash'had yatabuni mtandao wa wanachuo

11:59 - December 22, 2010
Habari ID: 2051500
Kufanyika kwa mafanikio duru ya tatu ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Wanachuo Waislamu kunaweza kuandaa uwanja unaofaa wa kudumishwa mawasiliano kati yao na hivyo kupelekea kubuniwa mtandao imara na madhubuti wa wanachuo wa Kiislamu duniani.
Akizungumzia suala hilo katika mahojiano na shirika la bahari za Qur'ani IQNA, Muhammad Baqir Khorramshad, Mkuu wa Taasisi ya Utamaduni na Uhusiano wa Kiislamu amesema kuwa mtandao kama huo unaweza kuwa na nafasi muhimu katika kufikiwa malengo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika pembe tofauti za dunia.
Huku akisema kuwa Qur'ani Tukufu ni ujumbe wa Mwenyezi Mungu ambao hupenya na kukaa imara kwenye nyoyo za vijana wanachuo, Khorramshad amesisitiza kuwa mipango madhubuti inapasa kutekelezwa kwa lengo la kufanya ujumbe huo ukite mizizi kwenye nyoyo hizo ambazo ziko tayari kuupokea ujumbe huo. Amesema mashindano ya Qur'ani ni moja ya njia bora zaidi za kueneza mafundisho na utamaduni wa Kiislamu duniani.
Akiashiria kuwa wanachuo ni sehemu muhimu ya jamii ya mwanadamu, Khorramshad amesema kuwa uandaliwaji wa mashindano hayo unaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuzima njama za maadui na vyombo vya habari vya kibeberu dhidi ya Uislamu, Ushia na malengo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ameashiri kufanyika duru ya tatu ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Wanachuo Waislamu katika mji mtakatifu wa Mash'had na kusema kuwa vitengo vya utamaduni vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi za nje vina nafasi muhimu katika kuchagua washindani wanaofaa wa mashindano hayo. 716457
captcha