Ayatullah Sayyid Abdallah al-Ghureifi, mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa kidini nchini Bahrain amesema kuwa taasisi zenye chuki na agenda za siri dhidi ya Ushia ndizo zilizoeneza tuhuma na uvumi wa hivi karibuni dhidi ya Ayatullah Ali Sistani wa nchini Iraq kwa lengo la kuchafua itibari na jina la mwanazuoni huyo mashuhuri wa kidini.
Huku akitoa taarifa kuhusiana na propaganda sumu zinazoenezwa dhidi ya Ayatullah Sistani, al-Ghureifi ambaye ni mwanafunzi wa Shahid Sayyid Ayatullah Muhammad Baqir Swadr, amesema kuwa madai yaliyotolewa hivi karibuni na Donald Rumsfeld, Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Marekani kwamba nchi hiyo ilimpa Ayatullah Sistani dola milioni 200 kwa lengo la kurahisisha uvamizi wa Iraq na kutoa fatuwa inayoharamisha kuuawa askari wa Marekani nchini humo ni uwongo mtupu na kwamba lengo lake ni kueneza dharau ya moja kwa moja dhidi ya taasisi muhimu ya umarja' wa kidini. Amesema kuwa taasisi na jumuiya zenye chuki na uadui dhidi ya Uislamu na umarja' wa kidini ndizo zinazoeneza propaganda hiyo sumu na kwamba vyombo vya habari vilivyo na chuki dhidi ya umarja' wa kidini pia vimechangia sehemu kubwa katika kueneza uvumi huo usio na msingi.
Ayatullah al-Ghureifi ameongeza kwamba umma wa Kiislamu umejifunza kwamba unapasa kusimama na kutetea thamani za kidini na maulama wa Kiislamu wanapolengwa na chuki na dharau ya maadui. Ameongeza kwamba maadui wa Uislamu wamekuwa wakifanya propaganda na njama za kuzusha hadhi ya umarja' unaopambana na ubeberu unaotaka kupora mali na maliasili ya nchi za Kiislamu. 720318