Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) inapanga kuchunguza hali ya Wakristo katika Mashariki ya Kati katika kikao chake kilichopangwa kufanyika tarehe 19 mwezi huu wa Januari huko Abu Dhabi, mji mkuu wa Imarati.
Kwa mujibu wa pendekezo lililotolewa na Nabih Berrih, Spika wa Bunge la Lebanon, kikao kikuu cha OIC huko Abu Dhabi kinatazamiwa kuchunguza hali ya Wakristo katika Mashariki ya Kati na njia za kulinda haki zao na vilevile jinsi ya kukabiliana na njama za utawala haramu wa Israel za kuyahudisha Quds Tukufu na kulinda utambulisho wa Kiislamu wa mji huo mtakatifu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Berrih, kikao hicho pia kimepanga kuchunguza matukio ya hivi karibuni ya Iraq na shambulio la bomu lililotokea karibu na kanisa la al-Qiddissin katika mji wa Alexandria huko Misri.
Taarifa hiyo imesema nafasi ya OIC katika kuwalinda wafuasi wa dini za wachache wanaoishi katika nchi za Kiislamu ni jambo muhimu litakalopewa uzito katika kikao cha Abu Dhabi. 723997