IQNA

Mahafidh wa Qur'ani wana nafasi na majukumu muhimu katika jamii

14:32 - January 11, 2011
Habari ID: 2062694
Mahafidh wa Qur'ani Tukufu wana nafasi na majukumu muhimu na jamii ina matarajio makubwa kutoka kwao.
Hayo yamesemwa na Yassin Mamduh al-Hamui mwakilishi wa Syria katika duru ya tatu ya mashindano ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu yanayofanyika katika mji mtakatifu wa Mash'had, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa shirika la habari za Qur'ani la IQNA. Amesema mahafidh wa Qur'ani wanapasa kuwa na tabia na maadili bora na kutekeleza kikamilifu mafundisho ya kitabu hicho kitakatifu maishani. Amesema, maadili ya Qur'ani hayapasi kukomea kwenye jamii tu kwa sababu kitabu hicho kinatutaka tuwe na tabia njema hadharani na faraghani.
Al-Hamui ambaye ni mwanachuo wa mwaka wa tano anayesomea tiba katika Chuo Kikuu cha Damascus amesema kuwa Qur'ani humpa moyo na msukumo mkubwa wa kufanya mambo mema katika maisha yake ya kila siku. Ameongeza kuwa Qur'ani imekuwa ngao, tegemeo na nguzo yake muhimu katika hali ngumu maishani.
Al-Hamui amesema kumtegemea Mwenyezi Mungu na msaada wa wazazi wake ni mambo mawili muhimu ambayo yamemsaidia sana katika kusoma na kufanikiwa kuhifadhi Qur'ani nzima.
Hii ni mara ya kwanza kwa mwanachuo huyo aliye na umri wa miaka 22 na aliyehifadhi Qur'ani nzima kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya wanachuo wa Kiislamu, katika nafasi hiyo. Katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu yaliyofanyika mjini Dubai mwaka 2009, mwanachuo huyo alishika nafasi ya nne. 728006
captcha