Kwa amujibu wa gazeti la ad-Dastur la Misri taasisi iliyotajwa iliandaa kikao cha dharura siku ya Alkhamisi, kilichosimamiwa na Ahmad Tayyib, Sheikh wa al-Azhar, kwa shabaha ya kuchunguza uhusiano wa pande mbili hizo na kuchukua uamuzi wa kusimamisha kwa muda usiojulikana uhusiano uliokuwepo kutokana na matamshi ya dharau ya mara kwa mara yanayotolewa na Papa Benedict wa XVI dhidi ya Uislamu.
Taarifa iliyotolewa mwishoni mwa kikao hicho imesema kuwa uchokozi wa aina zote dhidi ya wasio Waislamu unakemewa na mafundisho ya Kiislamu na kwamba dini hiyo hairuhusu hata kidogo kuhatarishwa maisha yao.
Hitilafu zilizojitokeza hivi karibuni kati ya Waislamu na Wakristo wa Misri zimempelekea Papa Benedict kutoa matamshi yasiyofaa dhidi ya Uislamu ambayo yamekuwa yakijibiwa na shakhsia mbalimbali wa kidini wa Misri, wakiwemo wa al-Azhar.
Al-Azhar imekuwa na kamati maalumu ambayo kila mwaka hufanya vikao na viongozi wa kidini wa Vatican kwa shabaha ya kufuatilia mazungumzo ya kidini na kuimarisha uhusiano wa pande mbili. 734212