IQNA

Kasisi aliyeivunjia heshima Qur'ani azuiwa kuingia Uingereza

10:14 - January 23, 2011
Habari ID: 2068982
Serikali ya Uingereza imetangaza kuwa imekataa kumpa viza ya kuingia nchini humo kasisi wa Kimarekani Terry Jones aliyezusha malalamiko makubwa kote duniani baada ya kutishia kuchoma moto kitabu kitakatifu cha Qur'ani katika kumbukumbu ya matukio ya Septemba 11 nchini Marekani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza amesema serikali ya London inapinga misimamo mikali na kwa sababu hiyo imekataa kutoa viza kwa Kasisi Terry Jones ambaye imesema amekuwa akitoa matamshi yanayoakisi mwenendo wake usiokubalika. Amesema kuwa Uingereza hairuhusu watu kama hao ambao hawahudumii maslahi ya taifa kuingia nchini humo.
Jumuiya ya watu wanaopinga wahajiri wa kigeni ilikuwa imemwalika Kasisi Terry Jones kutembelea Uingereza. Hata hivyo kundi linalopinga misimamo mikali limeitaka serikali ya London kumzuia kasisi huyo asiingie nchini humo kutokana na misimamo yake ya kibaguzi dhidi ya dini ya Kiislamu hususan Kitabu Kitakatifu cha Mwenyezi Mungu Qur'ani. 734630
captcha