Sheikh Nabil Qawuq, Naibu Mkuu wa Baraza la Utendaji la Chama cha Mapambano ya Kiislamu cha Lebanon Hizbullah ameashiria kudhoofika kwa ushawishi wa Marekani katika Mashariki ya Kati na kusema kuwa hatua ya nchi hiyo ya kukabiliana moja kwa moja na harakati ya mapambano ya Walebanon ni ishara ya wazi kuwa nafasi ya nchi hiyo katika eneo hili inazidi kudhoofika.
Amesema kila hatua inayochukuliwa na Marekani kwa ajili ya kuathiri uamuzi wa mahakama ya kimataifa inayoshughulikia mauaji ya Rafiq Hariri Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon dhidi ya Hizbullah haitakuwa na athari yoyote wala kuathiri azma ya harakati hiyo ya kupambana na uchokozi wa Wazayuni dhidi ya Lebanon.
Huku akisisitiza kwamba harakati hiyo ya Kiislamu imesimama imara mbele ya njama zote za Wamarekani na Wazayuni, Sheikh Qawuq amesema kuwa Marekani inaweza kuchukua uamuzi wowote katika miji mikuu ya Magharibi kwa maslahi yake lakini kwamba haiwezi kufanya hivyo ndani ya mipaka ya Lebanon.
Amesisitiza kwamba Marekani daima itaendelea kuwa dhaifu nchini Lebanon na kwamba wananchi wa nchi hiyo hawataruhusu nchi yao kutumiwa kama uwanja wa kufuatiliwa na kudhaminiwa malengo haramu ya Wamarekani katika Mashariki ya Kati. 735517