Abdalla al-Mubarak, mkuu anayesimamia masuala ya Qur'ani Tukufu na utafiti wa Kiislamu katika Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Kuwait ametangaza habari ya kufunguliwa kituo cha Qur'ani cha al-Wiqayan nchini humo mwezi Machi mwaka huu.
Kwa mujibu wa gazeti la Kuwait la al-Qabas, hiyo itakuwa taasisi ya kwanza kuasisiwa na kamati andamizi inayofuatilia masuala ya mikataba ya kukarabati na kuhifadhi Qur'ani Tukufu na utafiti wa Kiislamu ya Kuwait. Amesema, Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu imeahidi kuendelea kusaidia shughuli za Qur'ani nchini Kuwait kwa kuchangia ujenzi, ustawi na hifadhi ya vituo na taasisi za mafunzo ya Qur'ani.
Kwa kutilia maanani kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaofuatilia masuala ya Qur'ani, Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Kuwait imeazimia kuongeza vituo vya mafunzo ya Qur'ani. Kuhusiana na suala hilo baraza la mawaziri la Kuwait limeafiki kujengwa vituo na taasisi zaidi za Qur'ani nchini humo.
Akiashiria juhudi zinazofanywa na wahisani wa masuala ya Qur'ani nchini Kuwait, al-Mubaraka amesisitiza kuwa jambo hilo linabainisha jitihada zinazofanywa na Wakuwait kwa ajili ya kueneza mafunzo ya Qur'ani ndani na nje ya nchi hiyo. 739381