Akizungumzia suala hilo Iftikhar Abbas mkuu wa kamati hiyo amesema kuwa Karbala ina uwezo wa kubadilika na kuwa eneo muhimu zaidi la utalii ulimwenguni kutokana na kuwa na athari nyingi za historia na mambo ya kale. Amesema mkoa na mji mtakatifu wa Karbala una zaidi ya maeneo 200 ya mambo ya kale na athari za kuvutia za kihistoria ambazo baadhi zinarejea katika zama za kabla ya kudhihiri Uislamu. Amesema mengi ya maeneo hayo ya kuvutia hadi sasa hayajatembelewa na watalii wa kigeni kutokana na ukosefu wa usalama katika mikoa mingi ya Iraq na pia kutotangazwa ipaswavyo maeneo hayo kwa ajili ya kuwavutia watalii. Iftikhar Abbas amesema kuwa kamati iliyotajwa mwanzoni ya Karbala inafanya juhudi kubwa za kuyatangaza maeneo hayo kupitia televisheni za satalaiti ili kuwafahamisha walimwengu utajiri mkubwa wa mambo ya kale na vilevile turathi za kiutamaduni na kidini za Iraq.
Amesema kamati hiyo inashirikiana na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO kwa madhumuni ya kujengwa hoteli kubwa ya watalii katika mji wa Karbala kupitia uwekezaji wa kigeni.
Abbas ameongeza kuwa mji mtakatifu wa Karbala unahitaji kuwa na zaidi ya hoteli 200 kwa ajili ya kuwahudumia wafanyaziara wa Kiislamu na watalii wa kigeni ambao katika siku ya Arbaini iliyopita walikuwa kati ya watu laki tatu na nusu hadi laki nne na nusu. 740231