Kwa mujibu wa tovuti ya RUVR televisheni hiyo ambayo mipango ya kuianzisha ilianzishwa na serikali ya Russia miaka mitatu iliyopita kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa wafuasi wa dini tofauti nchini humo, ilianza kurusha hewani vipindi vyake vya majaribio hapo siku ya Jumapili.
Rais Dmitry Medvedev wa Russia, awali alikuwa amesisitiza umuhimu wa kuanzishwa televisheni hiyo na kusema kuwa lengo lake ni kurekebisha mtazamo wa Warussia kuhusiana na Uislamu. Amesema wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu wanapasa kusimamia uendeshaji wa televisheni iliyotajwa. Televisheni hiyo ya satalaiti itahudumia Waislamu wapatao milioni 20 ambao ni moja ya saba ya wananchi wote wa Russia.
Vipindi mbalimbali vitakuwa vikitangazwa kupitia televisheni hiyo kwa lengo la kuwanufaisha Waislamu na wasio Waislamu wa matabaka tofauti nchini humo.
Waislamu wanataraji kwamba televisheni hiyo itachangia pakubwa katika kupunguza mielekeo na fikra za chuki za baadhi ya makundi ya nchi hiyo dhidi ya Waislamu na Uislamu. 747159