IQNA

Mapinduzi ya Kiislamu, kigezo kwa mataifa ya Waislamu

11:35 - February 19, 2011
Habari ID: 2082817
Khatibu wa sala ya Ijumaa Tehran amesema kuwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kigezo cha mwamko wa Kiislamu katika mataifa mengine ya Kiislamu duniani.
Akihutubia halaiki kubwa ya waumini katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran, Ayatullah Ahmad Jannati ameongeza kuwa maandamano ya wananchi Wairani tarehe 11 Februari kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa 32 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yalikuwa ujumbe uliojaa nuru kwa mataifa mengine ya Kiislamu.
Khatibu wa sala ya Ijumaa ya Tehran ameashiria pia maandamano ya wananchi wa Yemen na Bahrain na kuwausia watawala wa eneo la Mashariki ya Kati kwamba, wawajali wananchi na kuzingatia matakwa yao na waache kudhamini matakwa ya mabeberu.
Wakati hayo yakiripotiwa wananchi wa Iran jana waliandamana nchi nzima baada ya sala ya Ijumaa kuwalaani wafanyaji fitna na uchochezi na kutaka viongozi wa wafanya fitna wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
Wananchi wa mjini Tehran pamoja na wa miji mingine ya Iran waliandamana baada ya sala ya Ijumaa kulaani ghasia za tarehe 14 Februari na wafanyaji fitna na kutoa nara dhidi ya Marekani, Israel na wanafiki. Pia wametaka kushtakiwa viongozi wa wafanyaji fitna na wanaowaunga mkono.
Kwingineko, Khatibu wa sala ya Ijumaa ya jana mjini Tehran ametaka viongozi wa tapo la uchochezi na fitna hapa nchini watiwe mbaroni. Huku akiashiria ghasia zilizotokea Jumatatu ya tarehe 14 Februari hapa mjini Tehran, Ayatullah Ahmad Jannati amesema kuwa, viongozi wa tapo la uchochezi na fitna walioshindwa katika uchaguzi wa Rais wanapaswa kuwekwa katika vizuizi vya nyumbani bila kuwa na suhula za kuwasiliana na ulimwengu wa nje kama vile simu na intaneti, ili wasiweze kutoa matamshi ya kuhadaa umma na kuzusha ghasia na machafuko nchini.
749782

captcha