IQNA

Wiki ya Kitaifa ya Qur'ani yaanza Algeria

16:25 - February 22, 2011
Habari ID: 2084849
Shughuli za kuadhimisha duru ya 12 ya Wiki ya Kitaifa ya Qur'ani zilianza jana Jumatatu katika kituo cha kidini cha Dar al-Imam katika mji wa Algiers nchini Algeria.
Kwa mujibu wa gazeti la nchi hiyo la an-Nahar al-Jadid, shughuli hizo zinazosimamiwa na Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kidini ya Algeria, zitajumuisha usomaji, hifdhi na tafsiri ya Qur'ani pamoja na hotuba zitakazotolewa na wanazuoni wa kidini kuhusiana na udharura wa kushirikishwa wanazuoni wa Algeria katika kuimarisha umar'ja wa kidini katika nchi za Kiarabu za kaskazini mwa bara la Afrika. Hotuba ya Rais Abdul Aziz Bouteflika wa nchi hiyo imesomwa katika ufunguzi wa wiki hii ya Qur'ani na mshauri wake Muhammad Ali Boughazi.
Rais Bouteflika amewashukuru wanazuoni wote walioshiriki katika sherehe za ufunguzi wa wiki hii na kusema kwamba kusadifiana kwake na siku ya kuzaliwa Mtume ni bishara njema kwa Waislamu wa nchi hiyo.
Rais wa Algeria amewashukuru pia wanazuoni wa Algeria kwa kuchangia pakubwa katika kuimarisha nafasi ya fiqhi, tafsiri ya Qur'ani na masomo mengine ya kidini nchini humo.
Wanafunzi na wanchuo wanashiriki katika mashindano mbalimbali ya Wiki ya Kitaifa ya Qur'ani ambapo washindi watapewa vibali vya kuiwakilisha nchi hiyo katika mashindano ya kimataifa ya usomaji na hifdhi ya Qur'ani Tukufu.
Wanafikra na wasomi wa Kiislamu pia watatoa hotuba katika vikao mbalimbali vya wiki hii kuhusiana na masuala tofauti yanayouhusu ulimwengu wa Kiislamu na uimarishwaji wa nafasi ya fiqhi na itikadi ya Kiislamu. 751705
captcha