Imesema kuwa vitendo hivyo vya kuua na kuwajeruhi wananchi wasio na hatia vinavyotekelezwa kwa madhumuni ya kuzusha hofu na woga miongoni mwao ni maafa ya kibinadamu.
Kwa mujibu wa gazeti la al-Yaum as-Sabe' Ekmeleddin Ihsanoglu Katibu Mkuu wa OIC amesema kuwa kuuawa na kujeruhiwa waandamanaji pamoja na kuzusha hofu miongoni mwao ni jambo linalokwenda kinyume na thamani za dini tukufu ya Kiislamu na hata za kibinadamu. Ameutaka utawala wa Libya kusimamisha mara moja mauaji na ukandamizaji huo na kufanya juhudi za kutatua matatizo na tofauti zilizopo kwa njia ya amani.
Huku akisema kuwa kubainishwa malalamiko na matakwa ya wananchi kwa njia ya amani ni haki ya kimsingi ya kila taifa, Ihsanoglu amesema kuwa kila nchi mwanachama wa OIC inapasa kuheshimu maazimio na sheria za jumuiya hiyo kuhusiana na masuala ya utawala, kuheshimiwa haki za binadamu, kushirikishwa makundi mbalimbali ya wananchi serikalini, kupambana na ufisadi pamoja na kukabiliana kwa amani na migogoro ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. 752358