IQNA

Sherehe za Milad-un-Nabii zaanza Lamu, Kenya

10:54 - February 28, 2011
Habari ID: 2087474
Maelfu ya Waislamu wa Kenya na kutoka maeneo mbali mbali duniani wanakusanyika katika Kisiwa cha Lamu kwa ajili ya sherehe za kila mwaka za kuadhimisha kuzaliwa Mtume Muhammad SAW zinazoanza Jumatatu Februari 28 had Ijumaa Machi 4.
Mratibu wa Msikiti wa Riadha na Kituo cha Kiislamu Lamu Sheikh Mohdhar Khitamy amesema Maulidi ya mwaka huu ambayo ni ya 125 yatahudhuriwa pia na wageni kutoka Visiwa vya Comoro, Yemen, Oman, Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia , Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Tanzania na Uingereza.
Ameongeza kuwa karibu Waislamu 25,000 wanatazamiwa kushiriki katika Maulidi ya mwaka huu.
‘Kuna kambi ya matibabu ya bure katika eneo la Msikiti wa Riadha na vilevile wafanyakazi wa afya 100 waliojitolea kutoka Kenya, Uhispania na Uingereza ambao watatoa huduma kwa wanaoshiriki katika Maulid’, amesema.
Sheikh Khitamy amesema wanazuoni wa Kiislamu kutoka Uingereza, Tanzania, Umoja wa Falme za Kiarabu na Kiongozi Mkuu wa Kiislamu wa Comoro Sheikh Said Twaher Jamal pamoja na Kadhi Mkuu wa Uganda ni kati ya watakaoshiriki katika Maulid hiyo.
‘Maulamaa hao watakuwa na warsha ya Kiislamu kwa viongozi wa jamii za Waislamu kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika’ amesema Sheikh Khitamy.
Ameongeza kuwa Maimamu kutoka kote nchini Kenya watashiriki katika kongamano kuhusu usimamisi wa Kiislamu katika majimbo yao. Aidha watajadili mbinu za kupambana na ugaidi. Mbali na Sherehe za Milad un Nabii zitakazojumuisha mihadhara ya kidini, mashindano ya Qur'ani na ibada za usiku, vilevile kutakuwa na tamasha za kiutamaduni.
754585
captcha