IQNA

Ayatullah Ali Khamenei:

Mwaka huu ninaupa jina la “Mwaka wa Jihadi ya Uchumi”

16:07 - March 21, 2011
Habari ID: 2097760
Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu “Ewe Mola unayebadili nyoyo na macho ya watu. Ewe Mola unayefanya tadbiri ya usiku na mchana. Ewe Mola unayebadilisha mwaka na hali za watu, badili hali zetu na kuzifanya bora zaidi.”
Ninatoa mkono wa baraka na fanaka za mwaka mpya na sikukuu ya Nairuzi kwa wananchi wote, Wairani wanaoishi katika maeneo mbalimbali duniani na mataifa mengine yanayoheshimu na kusherehekea sikukuu hiyo. Ninatoa mkono makhsusi wa sikukuu ya Nairuzi kwa watu na familia zinazohudumia nchi hii, Mapinduzi ya Kiislamu na utawala wa Kiislamu hapa nchini. Vilevile ninatoa mkono wa sikukuu ya Naiuzi kwa familia za mashahidi, vilema wa vita na familia zao, familia za watu ambao wanajishughulisha na kazi nyeti na muhimu katika kipindi hiki na kuwa mbali na familia zao katika siku hizi za sikukuu ya Nairuzi. Ninatarajia kuwa kwa baraka zake Mwenyezi Mungu taifa la Iran litakuwa na mwaka mpya uliojaa baraka na neema na kufanikiwa katika medani zote.
Hata hivyo masaibu yanayowapata watu katika baadhi ya nchi kama Bahrain, Yemen na Libya yamevuruga sikukuu ya mwaka huu na kutuzuia kusherehekea idi hii kikamilifu. Ninamuomba Mwenyezi Mungu ayape faraja mataifa ya Bahrain, Yemen na Libya na kuwapa adhabu yake maadui wa mataifa hayo.
Idi na sikukuu ni alama ya harakati ya kimaumbile ya mwanadamu katika kipindi cha mwaka, mwezi, mchana na usiku, na kwa kuwa harakati hiyo inapaswa kuelekea kwenye ukamilifu na daraja za juu, kila sikukuu na idi ni kipindi cha mwanadamu kuanza marhala na awamu mpya.
Katika mwaka uliopita wa 1389 Hijria Shamsia taifa la Iran limefanikiwa kufanya kazi kubwa kwa baraka na taufiki ya Mwenyezi Mungu. Mwaka uliopita tuliupa jina la Mwaka wa Hima na Uchapakazi Zaidi. Inafurahisha kwamba kaulimbiu hiyo imetekelezwa kivitendo katika kipindi cha mwaka mzima. Ninaweza kudai kuwa hii ni miongoni mwa nara na kaulimbiu zilizopewa mazingatio na wananchi na viongozi na kutekelezwa zaidi kivitendo katika miaka ya hivi karibuni. Hakika taifa na serikali imefanya hima kubwa na kuchapakazi zaidi katika harakati hiyo iliyoendelea kwa kipindi cha mwaka mzima.
Tumeshuhudia kazi kubwa zilizotekelezwa na nguvu tatu kuu za dola hususan serikali katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita katika nyanja za uchumi, siasa, mahudhurio makubwa ya wananchi katika medani mbalimbali za kisiasa na kimapinduzi, katika medani za sayansi na teknolojia, siasa za nje na nyanja nyingine mbalimbali. Miongoni mwa kazi hizo kubwa ni kuanza kutekeleza suala muhimu na nyeti la kutoa ruzuku kwa uadilifu na ni matarajio kuwa mpango huo utapata mafanikio kamili, inshaallah.
Kwa ujumla ninahisi kuwa nchi yetu inapiga hatua nzuri katika njia ya maendeleo na ukamilifu. Harakati hiyo inayoshika kasi zaidi siku baada ya siku imetokana na juhudi kubwa za viongozi na taifa zima katika kipindi cha miaka mingi, lakini inafurahisha kwamba kadiri miaka inavyopita harakati hiyo inashika kasi zaidi. Kwa mfano katika medani ya uzalishaji elimu, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na vituo vya kitaalamu vya kimataifa, Iran imekuwa na hisa ya zaidi ya asilimia 11 katika maendeleo ya kisayansi na uzalishaji elimu duniani, ilhali Iran inaunda asilimia moja tu ya watu wote duniani. Hii ni katika hali ambayo nchi inayofuatia Iran katika eneo hili katika maendeleo ya sayansi na uzalishaji elimu imekuwa na maendeleo ya chini ya asilimia sita.
Kwa msingi huo tunashukuru Mwenyezi Mungu kwamba maendeleo ya nchi yetu katika nyanja mbalimbali yanaridhisha. Harakati hii yenye kasi kubwa inapaswa kudumishwa sambamba na kufanya juhudi na hima zaidi.
Jambo linaloshuhudiwa katika masuala ya taifa ambalo linapaswa kupewa mazingatio zaidi katika mwaka mpya wa 1390 Hijria Shamsia ni kwamba miongoni mwa kazi muhimu zaidi za maadui za kukabiliana na taifa na nchi hii ni masuala ya kiuchumi. Maadui hao wanafanya harakati kubwa pia katika nyanja za utamaduni, siasa na kufanya njama za kuhodhi elimu na sayansi, lakini njama hizo ni kubwa zaidi katika uwanja wa uchumi. Vikwazo vilivyotayatarishwa na maadui dhidi ya taifa la Iran au vile vinavyotekelezwa dhidi ya taifa hili vimewekwa kwa lengo la kukwamisha maendeleo ya nchi hii na kusimamisha kasi ya harakati hiyo. Matakwa hayo ya maadui hayakutimia na hawakufanikiwa katika vikwazo hivyo. Tadbiri na juhudi za viongozi na taifa zimebatilisha njama za maadui lakini wangali wanafuatilia maalengo yao.
Kwa msingi huo katika mwaka huu mpya tunapaswa kutilia maanani masuala muhimu ya nchi, mhimili mkubwa zaidi ukiwa ni masuala ya kiuchumi. Kwa utaratibu huo mwaka huu ninaupa jina la “Mwaka wa Jihadi ya Kiuchumi” na ninawataka viongozi wa nchi kuanzia Serikali, Bunge na sehemu nyingine zinazojishughulisha na masuala ya uchumi na vilevile wananchi azizi wafanye jihadi kubwa katika harakati za kiuchumi. Harakati za kawaida hazitoshi na kuna udharura wa kufanyika jihadi kubwa katika medani hiyo.
Mnajua kwamba sasa tunaingia katika mwaka wa tatu wa Mwongo wa Maendeleo na Uadilifu. Kumefanyika kazi nzuri katika uwanja wa maendeleo na kwa kiasi kikubwa katika suala la kutekeleza uadilifu. Hata hivyo harakati zetu zinapaswa kufanyika kwa njia ambayo mwongo huu utakuwa dhihirisho la maendeleo na uadilifu hapa nchini. Kwa bahati nzuri harakati inayoendelea sasa katika ulimwengu wa Kiislamu inamfanya mtu ahisi kwamba kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, mwongo huu utakuwa mwongo wa maendeleo na uadilifu kwa eneo zima la Mashaiki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.
Ninamuomba Mwenyezi Mungu alibariki na kulipa taufiki taifa azizi la Iran, viongozi na nyinyi vijana wenye hima na vipawa na ni matarajio yangu kwamba tutapata baraka za dua za Imam wa Zama (as). Tunawakumbuka pia kwa dua mashahidi azizi na Imam Khomeini na tunamuomba Allah alipe rehma, ufanisi na maghufira taifa la Iran kwa baraka za roho zao tukufu.
Wassalam alaykum wa rahmatullah wa wabarakatuh 765868


captcha