Askari wa utawala wa al Khalifa wanaoungwa mkono na watawala wa Saudi Arabia tangu kuanza kwa harakati ya mageuzi ya wananchi wamevunja misikiti na maeneo mengi ya ibada nchini Barhain na kuchoma moto nakala za Qur'ani Tukufu, suala ambalo limejeruhi na kuumiza mno hisia za Waislamu.
Watawala hao wanapaswa kufunguliwa mashtaka kwa tuhuma za kuvunjia heshima kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu.
Hayo yamesemwa na mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu wa Lebanon Mai al Khansaa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Muungano wa Kimataifa wa Kupambana na Kinga ya Kuhukumiwa. Ameongeza kuwa Kasisi Terry Jones wa Marekani ambaye alichoma moto Qur'ani Tukufu alikuwa mtu mwenye misimamo ya kufurutu ada na alifanya hivyo kwa ajili ya kupata sifa za watu. Kasisi huyo amefunguliwa mashtaka na kwa msingi huo watu waliohusika na vitendo vya kuvunjia heshima Qur'ani huko Bahrain pia wanapaswa kufikishwa mahakamani, amesisitzia al Khansaa.
Mwanasheria huyo wa Lebanon amesema taifa la Waislamu la Bahrain linaelewa kwamba kitendo cha askari wa utawala wa kifalme wa nchi hiyo cha kuvunjia heshima Qur'ani tukufu hakiwezi kupunguza hadhi ya kitabu hicho kitakatifu na kwa mujibu wa aya ya 9 ya suratul Hijr, Mwenyezi Mungu Mwenyewe ameahidi kuwa atakilinda kitabu chake.
Bi al Khansaa amesema matukio ya Bahrain ni ugaidi unaotekelezwa na serikali dhidi ya wananchi na kuongeza kuwa dhulma za utawala wa Aal Khalifa dhidi ya wananchi wa Bahrain zilianza miaka mingi iliyopita. 795669