Kituo hicho cha Kiislamu ambacho kinajumuisha msikiti wa Tarare ulio karibu na mji wa Lyon kilishambuliwa usiku wa Jumatano na watu walio na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu na kuteketezwa kwa moto.
Akizungumzia tukio hilo la kusikitisha Ammar Bada, mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Tarare amesema kuwa miezi kadhaa iliyopita pia nara za kibaguzi na chuki dhidi ya Uislamu ziliandikwa na watu wasiojulikana kwenye kuta za eneo hilo la ibada. Amesema katika kipindi hicho wakuu wa kituo hicho walichukua uamuzi wa kufuta maandishi na nara hizo za chuki ili kupunguza mvutano miongoni mwa wakaazi wa mji huo lakini kwamba tukio la Jumatano usiku ndilo lililokuwa baya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika mji huo dhidi ya jamii ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo nyumba ya imamu wa msikiti na pia ya msimamizi wa kituo kilichotajwa cha Kiislamu ambazo zilikuwa kwenye ghorofa ya pili ya kituo hicho zilichomwa na kuharibiwa vibaya katika tukio hilo la kusikitisha la kibaguzi. Polisi ya Tarare imeanzisha uchunguzi wa tukio hilo. 805916