IQNA

Kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Musa Kadhim AS

12:47 - June 28, 2011
Habari ID: 2145684
Leo ni Jumanne tarehe 25 Rajab 1432 Hijria, inayosadifiana na tarehe 28 Juni 2011 Miladia. Siku kama ya leo miaka 1249 iliyopita yaani tarehe 25 Rajab mwaka 183 Hijria, aliuawa shahidi Imam Mussa Kadhim AS mmoja wa viongozi wa Waislamu baada ya Mtume.
Alizaliwa mwaka 128 Hijiria katika eneo la Abwaa baina ya Makka na Madina na hadi alipofikia umri wa miaka 20 alikuwa akistafidi na mafunzo mbalimbali kutoka kwa baba yake Imam Swadiq (a.s). Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Mussa Kadhim AS alichukua wadhifa wa uimamu na kuanza kuwaongoza Waislamu. Zama za Uimamu wake zilisadifiana na kipindi cha kushamiri elimu na kuenea utamaduni wa Kiislamu sambamba na kukua uhusiano wa Waislamu na mataifa mengine. Pamoja na kufundisha, Imam Kadhim AS alikuwa akiendesha harakati za mapambano dhidi ya dhulma na madhalimu wa utawala wa Bani Abbas. Baada ya Harun Rashid kuona kuwa Imam Kadhim ni hatari kwa utawala wake wa kidhalimu, alimtia mbaroni na kumfunga jela na kisha akapanga njama za kumuua kwa kumpa sumu katika tarehe kama ya leo.
Sambamba na kutoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyouawa shahidi Imam Mussa Kadhim AS, tunakunukulieni moja ya semi mashuhuri za Imam huyo: ‘'Wenzo bora kabisa wa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu baada ya kumtambua ni swala, kuwatendea wema wazazi na kisha kujiepusha na husuda, kujiona na kujifakharisha."
816502
captcha