Bibi Hakima, shangazi wa Imam Hassan Askari AS naye alikuweko nyumbani kwa Imam ili kuonana na jamaa zake. Wakati alipoazimia kuondoka na kurejea nyumbani kwake, Imam Hassan Askari AS alimzuia akimwambia, shangazi yangu mpendwa, usiku wa leo usiondoke, baki nasi hapa nyumbani. Hakima alijibu akisema: Leo nimekaa nanyi sana hapa nyumbani, kwa nini huniruhusu kuondoka? Imam alimwambia, leo hapa nyumbani atazaliwa mtoto ambaye kupitia kwake, Mwenyezi Mungu ataijaza dunia elimu, imani, uongofu na nuru baada ya duni kujaa dhulma na maovu. Baada ya kusikia maneno hayo, Bi Hakima aliuliza kwa shauku na furaha: Mwana huyo mtukufu atazaliwa na Nargis? Imam alijibu: Naam, atazaliwa na Nargis.
Kwa karne nyingi ulimwengu unasubiri kudhihiri mwokozi wa ulimwengu aliyeahidiwa. Watu waliodhulumiwa wanasubiri kwa hamu kubwa kudhihiri mtukufu huyo ili aje aziburudishe nyoyo zao kwa upepo mwanana wa alfajiri iliyojaa nuru na kuondoa machovu katika nyoyo zilizochoka. Imani ya Imam Mahdi kwa upande mmoja inapuliza uhai mpya katika mwili wa jamii ya mwanaadamu na kwa upande wa pili, inatoa bishara njema ya kupatikana saada na utukufu wa mwanaadamu wakati jua hilo tukufu, yaani Imam Mahdi AS, litakapochomoza.
Imam Mahdi AS ni mwana wa Imam Askari AS kutoka kizazi cha Bwana Mtume Muhammad SAW. Mama yake ni katika wajukuu wa mfalme wa Roma ambaye aliolewa na Imam AS katika kisa cha ajabu. Imam Hassan Askari alilazimika kumlea kwa siri mwanawe huyo mtukufu ili kumuepusha na maadui. Mwenyezi Mungu alimpa hekima, elimu na uongozi akiwa bado mdogo. Imam Mahdi alighibu na kutoweka mbele za watu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kujiepusha na uadui mkubwa wa maadui. Tab'an kwa muda fulani alikuwa na mawasiliano na watu mahsusi lakini baadaye Mwenyezi Mungu Mtukufu alimjaalie aghibu na atoweke mbele ya macho ya watu kwa muda mrefu hadi leo hii na hadi atakapodhihiri tena kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hivi sasa miaka mingi imepita tangu alipoghibu tena mwokozi huyo wa ulimwengu na watu bado wanasubiri kwa hamu kubwa kudhihiri kwa mtukufu huyo ili aje ayape uhai mpya maisha ya dunia.
Bishara ya kudhihiri mwokozi wa ulimwengu imekuwepo katika kipindi chote cha historia. Mitume na Manabii wakubwa wa Mwenyezi Mungu waliziona kwa uwazi zaidi ishara na dalili za kudhihiri mwokozi wa ulimwengu, Imam Mahdi AS. Kiujumla ni kwamba, imani ya kuweko "Aakhiruz Zaman" yaani zama za mwisho za dunia ni kitu kisicho na shaka hata chembe katika dini zote kubwa duniani na hasa hasa katika dini tukufu ya Kiislamu na itikadi hiyo inahesabiwa kuwa ni miongoni mwa misingi mikuu ya dini. Baadhi ya aya za Qur'ani Tukufu zinabainisha wazi kwamba, bishara ya kudhihiri mwokozi wa ulimwengu imekuja pia katika vitabu vya Mitume waliotangulia. Miongoni mwa aya hizo ni aya ya 5 ya Suratul Ambiyaa inasema:
وَلَقَدْ كَتَبْنَا فِی الزَّبُورِ مِن بَعْدِ الذِّكْرِ أَنَّ الأَرْضَ یَرِثُهَا عِبَادِیَ الصَّالِحُونَ
Na hakika tulikwishaandika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema.
Aya hii inatoa bishara kuhusu mustakbali wa dunia na ulimwengu huu kwamba itafika wakati dunia itajaa maovu na dhulma, wakati huo Mwenyezi Mungu atatuma waja wake wema watairithi dunia na kusimamisha usawa na uadilifu ndani yake.
Kitabu cha Zaburi ya Daud kimekariri mara kadhaa bishara hii adhimu ambapo katika sehemu moja ya mistari ya Kitabu hicho, Mwenyezi Mungu anamliwaza na kumpoza Mtume Wake Daud AS akimwambia asihuzunishwe na waovu kwani waovu ni mithili ya majani watatoweka haraka, bali atawakali kwa Mwenyezi Mungu kwani wanaotawakali kwa Mwenyezi Mungu ndio watakaorithi dunia.
Katika Kitabu cha Zend au Zand cha Wazartoshti pia kumeashiria zama za kutoweka dhulma na ukandamizaji na dunia kurithiwa na waja wema. Kinasema kuwa, baada ya kuondoka dhulma, dunia itatawaliwa na kheri na ufanisi na mwanaadamu ataishi katika maisha ya kheri na baraka.
Hata katika vitabu vya Wahindu pia kumezungumziwa suala la kudhihiri mwokozi wa ulimwengu katika zama za mwisho za dunia. Miongoni mwa vitabu hivyo ni kile cha Mahabharata. Kitabu hicho kimeandika kwamba dini zote zinaamini kuwa mwisho wa kila kipindi cha historia, mwanaadamu huporomoka kimaanawi na kiakhlaki na kutokana na kuwa mwanaadamu kimaumbile na kidhati yuko katika kuporomoka na kuzidi kuwa mbali na chimbuko lake, yeye mwenyewe hawezi kupambana na mwenendo huu wa kuporomoka kimaanawi na kiakhlaki. Hivyo hakuna njia nyingine ila kudhihiri shakhsia mwenye sifa bora kabisa za kimaanawi ambaye anapata ilhamu kutoka kwenye chimbuko la Wahyi, ili aje auokoe ulimwengu uliojaa kiza, ujinga, mghafala, dhulma na ukandamizaji.
Wafuasi wa dini ya Kiyahudi ambao wenyewe wanajinasibisha na Nabii Musa Kalimullah AS, pia wamo katika kusubiri mwokozi wa ulimwengu. Vitabu vya Mayahudi katika vile Taurati, Injili na vitabu vingine vya Mitume wao, kumejaa habari za kudhihiri mwokozi wa ulimwengu.
Katika Vitabu vya Injili ya Agano Jipya kama vile Injili za Mathayo, Luka, Barnaba n.k, kumebashiriwa sana pia kudhihiri mwokozi wa ulimwengu katika Aakhiruz Zamaan, yaani zama za mwisho za dunia.
Amma na kusubiri kudhihiri kwa Imam wa Zama, Imam Mahdi AS nako kuna maana pana. Miongoni mwa maana hizo ni kutokinaika na hali waliyo nayo hivi sasa watu wanaosubiri. Mtu mwenye kusubiri kudhihiri Imam Mahdi AS anapaswa kujitayarisha kikamilifu kimaanawi na jamii ya mwanaadamu kiujumla kwa ajili ya kuingia kwenye kipindi hicho kitakachojaa uadilifu na kutenda mema. Wanaadamu wanapaswa kuiweka mbali haki isikurubiwe na hasa pepesi za batili. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aharakishe kudhihiri kwa mwokozi wa ulimwengu, ili aje aijaze dunia haki, uadilifu na ibada ya Mola Mmoja tu, bila ya kushirikishwa na chochote.
Tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba kwa maadhimisho ya kukumbuka siku alipozaliwa Imam Mahdi AS.
826447