Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa, kusimama kidete taifa la Iran dhidi ya ubeberu wa Marekani kumepelekea kutokea mwamko wa Kiislamu katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.
Ali Larijani ameashiria stratijia ya Marekani mkabala na Iran na kubainisha kwamba, kama leo Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamevuka milima na mabonde na kuwa imara basi sababu yake ni kusimama kidete wananchi wa Iran mkabala na siasa za kupenda makuu za serikali ya Washington.
Spika Larijani amesema kwamba, hakuna wakati ambao Marekani ilitaka demokrasia iwepo Mashariki ya Kati na kitu ambacho daima viongozi wa Washington wamekuwa wakikifuatilia ni kulinda maslahi yao tu.
Spika wa Bunge la Iran amekosoa siasa za kindumakuwili za Marekani na kusifu misimamo ya wananchi wa Misri mkabala na njama za Marekani na waitifaki wake. Larijani amesema bayana kwamba, demokrasia ya Marekani ni ile ambayo inadhamini maslahi yake na si vinginevyo.
828391