Baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu wanafanya jitihada kubwa za kuzuia kesi inayomkabili dikteta wa zamani wa Misri Hosni Mubarak kwani wanaelewa vyema kwamba kufikishwa mahakamani kiongozi huyo aliyeng'olewa madarakani kutawashajiisha zaidi wananchi wa nchi za eneo hili kufanya mapinduzi zaidi na kuwapandisha kizimbani viongozi vibaraka.
Hayo yamesemwa na mtafiti, mchambuzi na mwandishi wa Misri Ahmad Hilal na kuongeza kuwa mapinduzi yanayotokea katika nchi za Kiarabu na Kiislamu ni juhudi za kutaka kurekebisha hali ya mataifa ya eneo hili. Ameongeza kuwa historia imethibitisha kwamba pale mataifa ya Kiislamu yanapodhulumiwa na kuona dosari katika uendeshaji wa masuala ya nchi zao hufanya mapinduzi na mageuzi kama yale yanayoshuhudiwa sasa katika nchi za Kiarabu.
Ahmad Hilal amesema mwamko wa Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati ni matokeo na jibu la mataifa ya Kiislamu kwa satua ya Marekani na Israel katika baadhi ya nchi za eneo hili na Waislamu wa mashariki ya Kati wanaelewa kwamba mali na utajiri wao unaporwa na wakoloni na viongozi tegemezi kwa Marekani; kwa msingi huo wameamua kusimama kidete dhidi ya wakoloni na viongozi madhalimu.
Mchambuzi huyo wa Misri amesema nchi za Magharibi zinazotumia siasa za kindumakuwili katika masuala ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika zinafikiria maslahi yao tu. Ameongeza kuwa wanasiasa wa Magharibi ambao sera zao za kuzikalia kwa mabavu moja kwa moja nchi za Kiislamu zimeshindwa na kuwatia hasara kubwa sasa wameamua kutumia mbinu ya kuzidhibiti nchi za Kiislamu kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja kwa kueneza fikra zinazopingana na Uislamu ili kuweza kufikia maslahi yao. 835350