Kwa kweli wanazuoni hao wanaweza kutajwa kuwa waanzilishi wa umoja katika ulimwengu wa Kiislamu. Hayo yamesemwa na Ayatullah Muhammad Ali Taskhiri, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Kukurubisha pamoja Madhehebu ya Kiislamu katika mahojiano yake ya hivi karibuni na Shirika la Habari za Qur'ani IQNA hapa mjini Tehran.
Amesema licha ya kuwa mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq ni kituo muhimu cha kidini cha Mashia lakini kimekuwa katika mstari wa mbele wa kutaka uwepo umoja kati ya umma wa Kiislamu na kushughulikia kwa karibu masuala na changamoto muhimu za Ulimwengu wa Kiislamu ukiwemo mzozo wa Palestina na harakati za kupambana na uebebru duniani. Ayatullah Taskhiri ameendelea kusema kuwa wanazuoni wakubwa kama vile Marehemu Kashif al-Ghitwaa walishirikiana kwa karibu na wanazuoni wa al-Azhar katika kuanzisha Daru Taqrib na kushajiisha umoja na mshikamano kati ya Waislamu, na kwamba tokea wakati huo hadi sasa kituo muhimu cha elimu ya kidini cha Najaf kimekuwa katika mstari wa mbele wa kupigania umoja na ushirikiano katika ulimwengu wa Kiislamu.
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kukurubisha pamoja Madhebu ya Kiislamu ameongeza kuwa Najaf kimekuwa kituo muhimu cha utafiti na marejeo ya kidini kwa muda wa karne 10 na chimbuko na akiba kubwa ya historia na elimu. Ameendelea kusema kuwa mji wa Najaf una utajiri mkubwa wa historia na mapambano dhidi ya ukoloni wa Uingereza pamoja na Mawahabi walio na misimamo ya kupindukia mipaka, jambo ambalo amesisitiza kuwa ni somo muhimu kwa umma wa Kiislamu.
Sheikh Taskhiri amesema kwa kuzingatia historia kongwe ya Najaf kuna ulazima kwa viongozi na wanazuoni wa mji huo kufanya juhudi kubwa ili kuuarifisha zaidi kwa walimwengu. Ayatullah Taskhiri ameongeza kuwa pendekezo la Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ISESCO la kuarifishwa mji huo kuwa mji mkuu wa kiutamaduni wa ulimwengu wa Kiislamu katika mwaka wa 2012 ni hatua nzuri inayowalazimu wakuu wa mji huo kufanya juhudi maradufu za kuarifisha na kudhihirisha utajiri mkubwa wa kielimu na kiutamaduni wa mji huo mtakatifu. 840740