IQNA

Swala ya jamaa ya pamoja ya Shia na Suni yafanyika nchini Syria

17:34 - August 13, 2011
Habari ID: 2169867
Swala ya jamaa ya pamoja kati ya wafuasi wa madhehebu ya Shia na Suni ilisimamishwa Jumatano iliyopita nchini Syria kwa uongozi wa Ayatullah Sayyid Mujtaba Husseini, mwakilishi wa Ayatullahil Udhma Ali Khamenei, Kiongozi wa Mfumo wa Kiislamu wa Iran, nchini humo.
Baada ya kumalizika Swala hiyo, Ayatulla Mujtaba Husseini alisisitiza juu ya udharura wa kuimarishwa ushirikiano wa wanazuoni wa Kishia na Kisuni katika mazingira magumu ya hivi sasa.
Akizungumza mbele ya hadhara ya wanazuoni hao katika ofisi ya uwakilishi wa Kiongozi Muadhamu mjini Damascus, Ayatullah Husseini alisema kuwa mgogoro wa hivi sasa wa Syria unahitajia kuwepo ushirikiano na mashauriano zaidi kati ya wanazuoni wa madhehebu mawili hayo muhimu ya Kiislamu kwa ajili ya kutatua matatizo na changamoto zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu.
Akizungumza katika hadhara hiyo, Sheikh Alau Deen az-Za'tari, Mkuu wa Idara ya Fatuwa katika Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Syria pia amewatakia funga njema Waislamu na kusisitiza kuwa wanapasa kuimarisha umoja kati yao hasa katika mwezi huu mtukufu. Ameashiria uhusiano mzuri na wa kihistoria ambao umekuwepo kwa miaka mingi kati ya Iran na Syria na kusisitiza umuhimu wa kuzingatiwa misimamo imara ya nchi mbili hizi katika kurejesha amani na usalama nchini Syria.
Balozi wa Iran nchini Syria pamoja na viongozi wa ngazi za juu wa serikali na wasio wa serikali walishiriki katika hadhara hiyo. 841652
captcha