Ripoti za vyombo vya habari zinaeleza kuwa watu wasiopungua 23 wakiwemo raia kadhaa wameuawa katika mapigano yaliyotokea kati ya vikosi vya serikali na wapinzani katika eneo la Arhab kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Yemen San'a.
Arhab inajulikana kama medani kuu ya mapambano kati ya vikosi vya serikali na wapinzani wa utawala wa miaka 33 wa Ali Abdullah Saleh ambapo hivi karibuni eneo hilo limeshuhudia matukio kadhaa ya mapigano kati ya pande mbili. Akthari ya watu wa makabila ya eneo la Arhab ni waungaji mkono wa Jenerali Ali Mushin al Ahmar ambaye alijiunga na wapinzani baada ya kujitoa katika jeshi la serikali ya San'a.
Wakati huohuo makundi ya upinzani yenye silaha yenye mfungamano na makabila ya maeneo ya kusini ambayo kwa majuma kadhaa sasa yamekuwa yakishirikiana na vikosi vya usalama kupambana na watu wenye silaha hususan katika eneo la Abyan, siku ya Jumanne yaliwatia nguvuni askari saba wakiwemo raia wawili wa Saudi Arabia huko katika mji wa pwani wa Shaqarah ulioko kusini mwa nchi hiyo na kuwakabidhi kwa vikosi vya usalama vya Yemen.
Ripoti nyengine kutoka Yemen zinaeleza kuwa wapinzani wa Ali Abdullah Saleh bungeni walipanga kufanya kikao maalumu hapo jana kwa lengo la kutwaa hatamu za uongozi wa nchi kwa kuunda baraza la taifa kutokana na nchi hiyo kubaki bila kuwa na Rais. Hii ni katika hali ambayo juzi Jumanne, Ali Abdulla Saleh akiwa mjini Riyadh, Saudi Arabia alitoa hotuba iliyorushwa hewani na televisheni ya serikali ya Yemen na kuwatangazia wafuasi wake kwamba karibuni hivi ataonana nao huko San'a. Katika hotuba yake hiyo dikteta wa Yemen aliwakosoa wapinzani wake bungeni akiwaita kuwa ni watu wenye malengo na fikra finyu na kuwatuhumu kuwa wamepora sha'ar za vijana wanaoandamana kumtaka yeye Saleh ajiuzulu.
Katika radiamali ya kwanza iliyotolewa na Sultan al Atwani dhidi ya matamshi hayo ya Ali Abdullah Saleh, kiongozi huyo wa upinzani amesema lengo kuu la dikteta huyo la kutaka kurudi nchini ni kuitumbukiza Yemen katika vita vya ndani. Al Atwani amesisitiza kuwa kutokana na vitendo viovu alivyofanya huko nyuma Ali Abdullah Saleh amepoteza itibari ya kisheria ya kutawala, na kwa hivyo hawezi kuwa na nafasi tena ya kushiriki katika siasa za nchi hiyo.
Tokea mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu, wananchi wa Yemen wameanzisha mapinduzi ya kuung'oa utawala wa kidikteta wa Ali Abdullah Saleh na kumtaka kiongozi huyo aondoke madarakani bila masharti yoyote.
Hadi sasa mamia ya watu wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa kwenye mapigano kati ya vikosi vya usalama na wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
846123