IQNA

Kikao kuhusu Libya kufanyika Uturuki

21:29 - August 23, 2011
Habari ID: 2175502
Kundi la Mawasiliano kuhusu Libya limeitisha kikao cha kujadili hali ya Libya siku ya Alhamisi ijayo mjini Istanbul, Uturuki.
Kikao hicho kinatazamiwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa nchi za Marekani, nchi za Ulaya na waitifaki wao Mashariki ya Kati pamoja na taasisi kadhaa za kimataifa.
Wakati huohuo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amevitaka vikosi vitiifu kwa Muammar Gaddafi viache kumuunga mkono dikteta huyo haraka iwezekanavyo ili kufungua njia ya kukabidhiwa madaraka kwa amani. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa kuna ulazima wa kukomeshwa mapigano na machafuko haraka iwezekanavyo.
Ban Ki- Moon ameongeza kuwa hadi sasa ameshawasiliana na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, mwakilishi mwandamizi wa Umoja wa Ulaya na viongozi wa nchi nyingine duniani ili kushauriana juu ya hali ya hivi sasa nchini Libya na kwamba leo jioni atafanya mazungumzo na Rais wa Baraza la Usalama pamoja na wawakilishi wa nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza hilo.
Kwingineko Mkuu wa Baraza la Taifa la Mpito la Libya amesema ana matumaini kuwa Muammar Gaddafi atakamatwa akiwa hai na kushtakiwa na kuhukumiwa kwa uadilifu. Mustafa Abduljalil amesisitiza kwamba vikosi vya wanamapinduzi bado havijaudhibiti kikamilifu mji mkuu Tripoli na kuongeza kuwa vikosi hivyo bado havijafanikiwa kuliteka eneo la Bab al Azizyah ambalo liko chini ya ulinzi mkali wa vikosi vitiifu kwa Gaddafi.
Abduljalil amefafanua kuwa kutokana na hali ilivyo hivi sasa haiwezekani kusema kuwa mapigano ya Tripoli yamemalizika.


848277
captcha