Taarifa hiyo imesema ushindi huo umetokana na kusimama kidete Walibya katika miezi ya hivi karibuni.
Taarifa hiyo imesema, kimsingi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikiunga mkono mwamko wa watu wa Libya lakini wakati huo huo inapinga uingiliaji wa madola ya kigeni nchini humo.
Iran imetoa wito kwa watu wa Libya walinde umoja wao wa kitaifa na wazuie satua ya madola ya kigeni hasa madola ya kikoloni ambayo huko nyuma yalimuunga mkono Gaddafi lakini leo yanadai kuwa katika safu ya wanamapinduzi.
Wakati huohuo Spika wa Bunge la Iran Dakta Ali Larijani amewatumia ujumbe wananchi wa Libya akiwapongeza kwa kumuondoa madarakani dikteta wa nchi hiyo na kusema kuwa wananchi shujaa wa Libya wamethibitisha kwamba kipindi cha tawala za kidikteta na kiimla kimefikia ukingoni katika zama hizi za mwamko wa mataifa mbalimbali. Amesisitiza juu ya kuheshimiwa matakwa ya wananchi.
Dakta Larijani amesema katika ujumbe huo kwamba jua la ushindi wa harakati ya mwamko wa Kiislamu sasa limechomoza katika nchi ya Libya na kukamilisha matakwa ya wananchi.
Spika wa Bunge la Iran amesema, baada ya kuangushwa utawala wa kidikteta wa Muammar Gadafi kuna udharura wa kuundwa serikali itakayozingatia matakwa ya wananchi wa Libya ambayo pia itawashirikisha wanamapinduzi wa Kiislamu bila ya kuruhusu uingiliaji wa madola ya kigeni.
Amesema taifa azizi la Libya linaelewa vyema kwamba wakora wa kimataifa wanaoongozwa na Marekani hawana lengo jingine ghairi ya kupora utajiri na maliasili ya nchi hiyo na kwa msingi huo kupuuzwa uingiliaji wa nchi za kibeberu katika masuala ya Libya kutakuwa na hasara ambazo haziwezi kufidiwa.
848511