IQNA

OIC yalaani shambulizi la kigaidi Abuja

20:07 - August 27, 2011
Habari ID: 2177662
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ametoa taarifa akilaani shambulizi la bomu lililotokea karibu na makao ya Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja na kukitaja kitendo hicho kuwa ni jinai na kinachokinzana na thamani na mafundisho ya Kiislamu.
Ekmeleddin Ihsanoglu ametoa wito wa kusakwa watu waliohusika na shambulizi hilo na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo.
Mlipuko huo wa bomu uliotokea jana karibu na makao ya Umoja wa Mataifa mjini Abuja umesababisha vifo vya watu wasiopungua 18. shambulizi hilo limebomoa kabisa jengo lililokuwa na ghorofa 5 na kuvunja madirisha ya nyumba za kandokando yake. Jengo hilo lililobomolewa pia lilikuwa na benki na ofisi za wakala wa usafirishaji na idadi kubwa ya watu waliokuwa wakipata huduma katika ofisi hizo wamejeruhiwa.
Kundi linalojiita la kidini la Boko Haram limetangaza kuwa limehusika na shambulizi hilo. Kushadidi kwa mashambulizi ya Boko Haram dhidi ya vituo vya kijeshi na maeneo nyeti ya Nigeria katika miezi ya hivi karibuni kumeilazimisha serikali ya Abuja izidishe ulinzi na usalama katika medani kuu hususan huko kwenye mji wa Borno kaskazini mwa Nigeria.
Kundi la Boko Haram lilijitokeza katika medani ya kisiasa ya Nigeria Januari mwaka 2004 na kutambuliwa kwa jina la 'Taliban wa Nigeria'.
Miongoni mwa malengo makuu ya kundi hilo ni kuasisi serikali eti ya Kiislamu na kutekeleza sheria za kidini. 850238


captcha