IQNA

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran:

Mwamko wa Kiislamu unazidi kuimarika

11:03 - September 03, 2011
Habari ID: 2180138
Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amesema mataifa ya Waislamu yamefika katika medani ya mapambano dhidi ya istikbari yakitoa nara dhidi ya Marekani na Utawala wa Kizayuni wa Israel huku yakifuatilia malengo ya Kiislamu.
Akihutubia waumini kutoka matabaka mbalimbali za jamii katika Chuo Kikuu cha Tehran, Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim Seddiqi ameashiria wimbi linalozidi kuongezeka la mwamko wa Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kusema kuwa maandamano ya wananchi wa Misri mbele ya ubalozi wa Utawala wa Kizayuni mjini Cairo pamoja na nara zao dhidi ya Marekani na Israel ni ishara ya kuimarika harakati dhidi ya mfumo wa kibeberu duniani.
Ameashiria kujitokeza kwa wingi wananchi wa Iran na nchi zingine za Kiislamu katika Siku ya Kimataifa ya Quds na kusema harakati mpya imeibuka katika Siku ya Quds mwaka huu. Ameongeza kuwa wananchi wa Misri kwa mara ya kwanza wameshiriki katika maandamano ya Siku ya Quds tokea ulipoangushwa utawala wa kiimla wa Mubarak. Katika maandamano hayo Wamisri walitoa nara dhidi ya utawala haramu wa Israel.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran ameashiria suala la vikwazo dhidi ya Iran. Amesema maadui wa Iran hawajaweza kufikia malengo yao ya kuanzisha vita au kuibua hitilafu nchini Iran na kwa hivyo hawatafikia malengo yao kupitia vikwazo vya kiuchumi. Amesema taifa la Iran sasa limevunja njama za maadui na kupata fahari na ushindi.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran ameelezea masikitiko yake kuhusu njaa na ukame nchini Somalia na amewataka wananchi wa Iran kuendeleza ukarimu wao kwa kutuma misaada zaidi nchini Somalia.
captcha