Baada ya hapo askari hao waliwafungia mahujaji hao kwenye kumbi ambazo hazikuwa na hali nzuri ya hewa na hivyo kupelekea baadhi ya mahujaji waliokuwa na umri mkubwa kuzirai. Walioshuhudia tukio hilo la kusikitisha wanasema kuwa askari usalama wa Saudia Arabia waliwashambulia mahujaji hao walipoanza kupiga nara za Allahu Akbar kwenye uwanja huo wa ndege kulalamikia hali mbaya ya huduma na dharau waliyokuwa wakifanyiwa na maafisa wa uwanja wa ndege wa Jeddah.
Mahujaji hao walikuwa wakilalamikia hatua ya maafisa wa uwanja huo wa ndege ya kuwachelewesha kwenye uwanja huo kwa muda wa siku tatu bila kuwaandalia huduma zinazofaa za afya wala za umma. Wamelalamika kuwa maafisa hao waliamiliana nao kwa dharau tokea walipofika kwenye uwanja huo.
Wakati huohuo mamia ya Wamisri wamefanya maandamano mbele ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Cairo kulalamikia kuvunjiwa heshima mahujaji hao wa Misri na vilevile uingiliaji wa nchi hiyo katika masuala ya ndani ya Misri. Wanaharakati wa Misri wametaka kufanyika maandamano zaidi nchini humo dhidi ya watawala wa Saudia. 853388