IQNA

Mashia wa Misri wazingirwa na wafuasi wa Mubarak

12:40 - September 08, 2011
Habari ID: 2183545
Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Ahlul Bait mjini Cairo Misri amesisitiza kwamba Mashia wa nchi hiyo wangali wanaendelea kushinikizwa kisiasa, kijamii na kimadhehebu na wafuasi wa dikteta Hosni Mubarak ambaye aling'olewa madarakani hivi karibuni.
Akibainisha suala hilo katika mazungumzo yake na televisheni ya al-Alam, Muhammad ad-Dureini amesema kuwa katika kipindi cha utawala wa Mubarak Waislamu wa madhehebu ya Shia wa nchi hiyo walikuwa wakikandamizwa moja kwa moja na askari usalama wa Misri, lakini hivi sasa wanapata mashinikizo makubwa kutoka kwa watu wanaowakufurisha misikitini na katika maeneo mengine ya ibada, watu ambao hudhaminiwa kifedha na mabaki ya wafuasi wa dikteta huyo.
Ameitaka serikali kufuatilia jambo hilo kwa haraka na kuwafukuza katika maeneo hayo mabaki ya Mubarak na wakufurishaji ambao wanatumia vibaya jina la Uislamu kuwakufurisha Waislamu wenzao.
Muhammad ad-Dureini amesema watu hao ndio wanaoendesha mahakama haramu za kujasusi na kupepeleza itikadi za watu nchini Misri na kuongeza kuwa makundi ya wasalafi nchini humo ni hatari kubwa kwa mustakbali wa nchi hiyo.
Ad-Dureini ameendelea kusema kuwa, Misri inakabiliwa na hatari na njama kubwa ya ghasia zinazopangwa kuzushwa nchini humo na mabaki ya wafuasi sugu wa Mubarak. Amewataka Wamisri wote kuwa macho na kuepusha hali kama hiyo inayoweza kuhatarisha usalama wa nchi hiyo. 856704
captcha