Wakati huo huo Ehud Barak Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel amefanya mazungumzo na Leon Panneta Waziri wa Ulinzi wa Marekani na kutaka kulindwa ubalozi wa utawala huo huko Misri. Serikali ya muda ya Cairo pia imelazimika kuitisha kikao cha dharura kuhusiana na suala hilo.
Hakuna shaka kuwa kumeibuka mgogoro mkubwa katika uhusiano wa utawala wa Kizayuni na Misri baada ya kung'olewa madarakani utawala wa Hosni Mubarak. Pamoja na hayo, kuuawa wanajeshi watano wa Misri katika eneo la Sinai katika mashambulio ya anga ya wanajeshi wa Israel mwezi uliopita kumeweka wazi zaidi mivutano iliyopo katika uhusiano wa utawala wa Tel Aviv na Cairo. Ukweli wa mambo ni kuwa, hali ya mambo ya sasa huko Misri inatofautiana sana na ile ya wakati wa utawala wa dikteta Hosni Mubarak. Takwa kuu la kimsingi linalosisitizwa na wananchi wa Misri tangu baada ya ushindi wa mapinduzi nchini humo ni kukatwa uhusiano wa Cairo na utawala wa Kizayuni.
Ijumaa ya jana ambayo ilipewa jina la "Siku ya Kubadilisha Mwelekeo," wananchi wa Misri walisisitiza juu ya matwaka yao kwa ajili ya kubadili mkondo wa mapinduzi na kulitaka Baraza Kuu la Kijeshi la nchi hiyo kumfukuza balozi wa utawala wa Kizayuni nchini humo na vilevile kufuta mkataba wa Camp David. Nukta muhimu ni hii kwamba, katika kuonyesha chuki na hasira zao kwa Israel, maelfu ya Wamisri jana walifanya shambulio la kimapinduzi na kuuharibu ukuta uliokuwa ukiuzunguka ubalozi wa utawala wa Kizayuni huko mjini Cairo Misri. Hatua hiyo ya wananchi wa Misri inadhihirisha wazi hasira na chuki kubwa waliyonayo kwa Israel.
Hali ya hatari imetangazwa kote nchini Misri hivi sasa kwa kuhofia kuibuka wimbi kubwa la maandamano ya raia wa nchi hiyo dhidi ya utawala wa Kizayuni. Pamoja na kuasisiwa uhusiano rasmi kati ya Misri na utawala wa Kizayuni tangu mwaka 1979, kufuatia kutiwa saini mkataba wa Camp David kati ya pande mbili hizo, lakini uhusiano huo haujavuka zaidi ya ngazi ya kiserikali. Wananchi wa Misri sambamba na fikra ya waliowengi katika eneo, wanauhesabu utawala haramu wa Kizayuni kuwa sawa na donda ndugu la saratani katika Mashariki ya Kati.
Hivi sasa ambapo mazingira mapya yamejitokeza huko Misri, wananchi wa nchi hiyo pia hawataki kupoteza muda na wanataka kuangaliwa upya uhusiano wa nchi hiyo na utawala wa Kizayuni. Kukatwa uhusiano na Israel, ambayo ni tishio kuu kwa nchi za eneo na khususan Misri, ni takwa kuu la wananchi wa Misri. Kuhusiana na suala hilo nukta iliyo wazi ni hii kwamba, viongozi wa utawala wa Kizayuni nao pia wamefahamu vyema kuwa, baada ya kuanza kwa wimbi la mapambano ya ukombozi ya Kiarabu katika baadhi ya nchi za eneo, zile nchi za Kiarabu ambazo ambazo awali zilikuwa bega kwa bega na na Israel, sasa zinaanza taratibu kujiweka mbali na utawala huo haramu.
Misri ya wakati wa utawala wa Mubarak ambayo ilikuwa dalali wa amani na siasa za Israel, sasa inakabiliwa na wimbi la hisia dhidi ya Uzayuni, wimbi ambalo limewaathiri pia viongozi wa utawala wa Kizayuni. Kwa kadiri kwamba Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala huo kwa hamaki amefanya mazungumzo ya simu na Rais Barak Obama wa Marekani na kumwomba ajaribu kutuliza hali ya mivutano iliyojitokeza kati ya Cairo na Tel Aviv.
857532