Huku akiashiria mwamko wa Kiislamu ambao unaonekana katika nchi kadhaa za Kiislamu na ulazima wa kuwepo umoja kati ya Mashia, Mkuu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq amesema kuwa kusimama imara mbele ya dhulma na uonevu ni jukumu muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele na Mashia wote duniani.
Akizungumza katika Kongamano la Tano la Kimataifa la Baraza Kuu la Ahlul Bait (as) linalofanyika mjini Tehran, Sayyid Ammar al-Hakim, Mkuu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq amesema kuwa katika hali tata ya hivi sasa Waislamu wa Kishia na wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) kote ulimwenguni wana majukumu mazito ambayo wanapasa kuyatekeleza. Amesema kulindwa na kuheshimiwa misingi ya kimaanawi na kiitikadi ya Ahlul Bait (as) pamoja na kufuatia mafundisho halisi ya watukufu hao mbali kabisa na imani potofu na vilevile kuhifadhi misimamo ya wastani katika hali tata inayotawala hivi sasa duniani ni miongoni mwa mambo muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele na wafuasi wa madhehebu ya Ahlul Bait (as).
Ammar al Hakim amesema vipaumbele vingine ni kusimama imara mbele ya dhulma na uonevu wa mabeberu, kuarifisha mafundisho ya Ahlul Bait (as) duniani na kuwafahamisha walimwengu amani ya kijamii inayohubiriwa na madhehebu hii muhimu ya Kiislamu. Amesema suala la Palestina ni jambo jingine muhimu linalowakabili Waislamu na kwamba kuwatetea Wapalestina kwa kila njia inayowezekana katika kukabiliana na dhulma wanayofanyiwa na Wazayuni wa Israel ni moja ya majukumu muhimu ya wafuasi wa Ahlul Bait (as).
Amesisitiza juu ya umuhimu wa kulindwa malengo ya mwamko wa Kiislamu unaoendelea katika nchi kadhaa za Kiarabu na kuwataka Waislamu wa nchi hizo wawe macho dhidi ya njama zinazofanywa na mabeberu kwa ajili ya kupotosha malengo ya mapinduzi yao.
Vilevile ameashiria hali ya Mashia wa Iraq na kusema kuwa wanashirikiana kwa karibu ili kufikia maendeleo na ustawi nchini. 858877