Mustafa Abdul Jalil, Mkuu wa Baraza la Mpito la Libya amesema kuwa dini tukufu ya Kiislamu itakuwa chanzo muhimu cha kubuniwa sheria nchini Libya baada ya kung'olewa madarakani dikteta Muammar Gaddafi.
Akizungumza mbele ya umati mkubwa katika Medani ya Mashahidi mjini Tripoli mara tu baada ya kuwasili katika mji huo hapo siku ya Jumatatu, Abdul Jalil amesema kuwa Walibya ni Waislamu na kwamba hawataruhusu kutawaliwa na sheria wala fikra nyingine yoyote isiyosimama juu ya msingi wa mafundisho ya Kiislamu.
Amesema kwamba Waislamu wa Libya ni Waislamu wenye misimamo ya wastani na kwamba wataendelea kuishi na kudumisha misimamo hiyo.
Abdul Jalil amesisitiza kwamba Walibya kamwe hawatatoa mwanya wa kutekwa nyara mapinduzi yao na maadui wasiowatakia kheri wananchi wa nchi hiyo. 859806