IQNA

Serikali ya Zanzibar yateua viongozi wa Kiislamu

7:21 - September 29, 2011
Habari ID: 2195276
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein ameteua viongozi wa dini ya Kiislamu akiwemo Mufti Mkuu pamoja na Kadhi Mkuu wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu 26 September, Saleh Omar Kabhi ameteuliwa kuwa Mufti Mkuu wa Zanzibar ambaye anachukua nafasi ya Harith bin Khelef aliyefariki dunia miaka miwili iliyopita nchini India akitibiwa.
Sheikh Kabhi pia ni kiongozi wa Baraza la Maulamaa Zanzibar, lenye uwezo wa kutoa kauli ya mwisho kuhusu masuala ya dini ya Kiislamu visiwani humo.
Aidha, Rais Dk. Shein amemteua Sheikh Khamis Haji Khamis kuwa Kadhi Mkuu wa Zanzibar.
Kabla ya uteuzi huo, alikuwa akikaimu nafasi hiyo kwa muda wa miaka minne kutokana na kifo cha Kadhi Mkuu Mussa Makungu.
Mufti pamoja na Kadhi Mkuu ndiyo viongozi wa ngazi za juu katika masuala ya mambo ya Kiislamu ikiwemo kutoa taarifa za kuandama kwa mwezi pamoja na kutoa fatuwa katika masuala yote yanayohusu mambo ya Kiislamu kama vile ndoa na waqfu.
Zanzibar ni eneo linalojitawala katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu asilimia 97 ya wakazi wa Zanzibar ni Waislamu.
869281
captcha