Spika wa Bunge la Iran Dakta Ali Larijani ambaye ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kikao cha mwisho cha mkutano huo amesema kuwa kutetea na kuunga mkono mapambano ya Palestina siku zote kumekuwa katika ajenda ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amekosoa mpango wa Mahmoud Abbas uliowasilishwa katika Umoja wa Mataifa na akasema mpango huo hauoani na mazingira ya sasa wakati utawala wa Kizayuni wa Israel umetengwa zaidi na mataifa ya Mashariki ya Kati nayaendelea kupata ushindi.
Kwa upande wake Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, harakati ya kukaliwa kwa mabavu Palestina na kuasisiwa dola ghasibu na bandia la Israel ni hatua iliyokuwa dhidi ya wanadamu wote. Rais Ahmadinejad amesema kuwa, kadhia ya Palestina ina umuhimu mkubwa na kwamba, kuna haja ya kuweko umoja na mshikamano katika kuunga mkono Intifadha ya Palestina. Dakta Ahmadinejad amesisitiza kuwa, matunda ya kusimama kidete wananchi madhulumu wa Palestina kwa miongo kadhaa yatapatikana tu kwa kuweko himaya na uungaji mkono wa nchi za Kiislamu na haipaswi kuwa na matumaini na mipango ya Kimagharibi kuhusiana na kadhia hii.
Rais wa Iran amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel na madola ya Magharibi yamefanya njama za kupotosha historia na kulifuta taifa la Palestina katika historia lakini kusimama kidete wananchi wa Palestina na mwamko wa Kiislamu Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika kumesambaratisha njama zao zote.
Taarifa ya mwisho ya mkutano huo imeitambua hotuba iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei katika ufunguzi wa mkutano huo kuwa ni hati rasmi ya mkutano huo. 862640