IQNA

Viongozi wa kidini kukutana kesho Italia

18:47 - October 26, 2011
Habari ID: 2212489
Viongozi wa kidini kutoka zaidi ya nchi 50 za dunia wanatazamiwa kukutana katika mji wa Assisi huko Italia hapo kesho Alkhamisi kutokana na mwaliko wa Papa Benedict XVI.
Viongozi hao wapatao 300 kutoka dini zote za mbinguni na zisizo za mbinguni watakutana katika mji huo ili kujadili njia za kupambana na vitendo vya utumiaji mabavu.
Viongozi hao wanatazamiwa kutangaza wazi msimamo wao wa kupinga tabia za baadhi ya watu kutoka dini zote za Kikristo, Kiislamu, Kiyahudi, Kihindu na zisizokuwa hizo kutumia jina la dini katika kuhalalisha na kudumisha vitendo vyao vya mabavu na ugaidi kwa jina la dini.
Washiriki wa kikao hicho watasali kwa mujibu wa sheria zao za kidini kama njia ya kuthibitisha kwamba dini zao zinapigania amani na uadilifu duniani.
Kikao hicho kinafanyika katika hali ambayo Sheikh wa al-Azhar nchini Misri, ambacho ni kituo muhimu cha kidini katika ulimwengu wa Kiislamu, alitangaza kwamba hatashiriki katika kikao hicho kutokana na msimamo wa upendeleo wa Papa Benedict aliouonyesha hivi karibuni wa kuwatetea Wakristo wa Kikopti wa nchi hiyo dhidi ya Waislamu katika machafuko ya hivi karibuni.
Katika kikao kama hicho ambacho kilifanyika mwaka 1986 ni wawakilishi kutoka nchi 11 tu ndio walioshiriki.
Wawakilishi kutoka nchi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia pia wanashiriki katika kikao cha mwaka huu. 887373
captcha