Bakirat amesema kuwa ameshangazwa kuona kwamba nuskha adimu za Qur'ani na maandishi mengine ya Kiislamu ambayo yameonyeshwa kwenye maonyesho hayo yanayofanyika katika Chuo Kikuu cha Kiebrania huko Quds zimetolewa katika nchi za Kiislamu kama vile Iraq. Amehoji ni vipi utawala ghasibu wa Israel ambao unatumia kila mbinu kuharibu athari na utamaduni wa Kiislamu katika ardhi unazozikalia kwa mabavu za Palestina umegeuka ghafla na kuwa mteteaji wa athari hizo kwa kuandaa maonyesho hayo?
Sheikh Najih Bakirat amesema Wapalestina hawatashirikiana kwa namna yoyote ile na utawala kama huo unaoiba na kupora athari za Kiislamu, na wakati huohuo kuutaka urejeshe nuskha hizo kwa wamiliki wake halisi haraka iwezekanavyo.
Wazayuni wanaoandaa maonyesho hayo wanadai kwamba lengo lao ni eti kujaribu kuwaonyesha watu utamaduni mzuri na wa thamani kubwa wa Kiislamu!
Wataalamu wa mambo wanaitakidi kwamba watawala wa Kizayuni wa Israel wameandaa maonyesho hayo ili kujaribu kufunika jinai na unyama wao dhidi ya Waislamu wa Palestina, na wakati huohuo kujaribu kujidhihirisha kuwa watu wanaotafuta amani na Wapalestina.
Watawala hao wameandaa maonyesho hayo ya kuwapumbaza walimwengu katika hali ambayo walowezi wa Kizayuni wanaoungwa mkono na jeshi la utawala huo kila siku hushambulia kinyama Wapalestina na kuharibu maeneo yao matakatifu, kukiwemo kuchoma moto misikiti yao na kuvunjia heshima kitabu chao kitakatifu cha Qur'ani. 890765