Gazeti la nchi hiyo la Sabq limeandika kuwa Sheikh Abdul Muhsin al-Abikan ambaye ni mshauri wa Halmashauri ya Kifalme ya Saudia amepinga vikali hatua iliyochukuliwa hivi karibuni na sheikh mwenzake Awadh al-Qarni ya kutoa zawadi ya dola laki moja kwa kila mtu atakayemteka nyara askari wa utawala ghasibu wa Israel kwa lengo la kubadilishana na mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za utawala huo.
Al-Abikan amedai kuwa hatua hiyo ni ukiukaji wa uwezo na mamlaka waliyopewa mashekhe na wanazuoni kwa sababu eti utekaji nyara wa aina hiyo unapasa tu kufanyika katika medani ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Amedai kwamba jambo hilo linakwenda kinyume kabisa na misingi ya sheria za Kiislamu, akili na misingi inayokubalika kwenye jamii na kwamba linahatarisha usalama wa Saudia na vilevile kuharibu jina la Waislamu duniani.
Awadh al-Qarni, sheikh wa Kiwahabi wa Saudi Arabia hivi karibuni alitangaza kuwa atatoa zawadi ya dola laki moja kwa kila Mpalestina atakayemteka nyara askari wa Kizayuni ili kubadilishana mateka huyo na mateka wa Kipalestina wanaoteseka kwenye jela za kuogofya za utawala ghasibu wa Israel.
Baada ya tangazo hilo Mwanamfalme Khalid bin Talal aliunga mkono msimamo wa sheikh huyo na kuongeza zawadi hiyo kwa dola laki tisa nyingine na hivyo kufanya zawadi hiyo kufikia dola milioni moja. 891833