IQNA

Muammar Gaddafi:

Kama utume usingehitimishwa nami ningekuwa mtume!

8:55 - November 03, 2011
Habari ID: 2216790
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Kijeshi na mshauri zamani wa dikteta aliyeuawa wa Libya Kanali Muammar Gaddafi amesema kuwa Imam Mussa Sadr aliuawa na kiongozi huyo wa zamani wa Libya.
Muhammad al Khidhar ameiambia televisheni moja ya Misri kwamba kiongozi huyo wa ngazi za juu wa kidini wa Lebanon aliuawa na Gaddafi ambaye alikuwa amemwalika nchini humo. Amesema alimsikia kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa utawala wa Libya akisema kwamba aliamrishwa na Gaddafi kumuua Imam Mussa Sadr.
Al Khidhar amesema sababu ya kuuawa kiongozi huyo wa kidini ni mjadala mkali uliojiri baina yake na Gaddafi kuhusu itikadi ya dikteta huyo wa zamani wa Libya ya kutaka kubadili baadhi ya aya za Qur'ani.
Mshauri wa zamani wa Gaddafi anasema, katika mjadala huo mkali dikteta wa Libya alisema: "Kama utume usingehitimishwa basi yeye pia angekuwa mtume!"
Mwendesha Mashtaka wa Kijeshi wa zamani wa Libya anasema, mjadala baina ya Gaddafi na Imam Mussa Sadr ulipamba moto zaidi baada ya maneno hayo ya Gaddafi na ndipo Imam Sadr alipomwambia kwamba ni kafiri. 'Gaddafi alikasirika mno na kuamuru Imam Mussa Sadr auawe' amesisitiza al Khidhar.
Amesema kuwa baada ya kuuawa Imam Sadr, vyombo vya usalama vya Libya vilichukua hatua ya kuficha mauaji hayo kwa kutuma mavazi yake nchini Italia.
Amesema kuuawa kwa dikteta Gaddafi kutatatiza kazi ya kuweka wazi zaidi picha halisi ya mauaji ya Imam Mussa Sadr. 891813
captcha