IQNA

Gaidi ajilipua katika swala ya Idul Adh'ha nchini Afghanistan

20:15 - November 06, 2011
Habari ID: 2218546
Gaidi mmoja amejilipua leo Jumapili katika swala ya Idul Adh'ha huko katika mkoa wa Baghlan nchini Afghanistan na kuua watu kadhaa na kujeruhi wengine.
Kwa mujibu wa televisheni ya al-Manar, mlipuko huo uliotokea masaa ya adhuhuri katika msikiti mmoja wa mkoa huo ulipelekea watu sita kupoteza maisha yao akiwemo polisi mmoja.
Vyambo vya kuaminika vinasema kwamba mlipuko huo ulitekelezwa na gaidi mmoja aliyekuwa amejifunga mada za milipuko na kujilipua katikati ya waumini waliokuwa wamemaliza kuswali na kuanza kuondoka katika msikiti uliotajwa. Vyombo hivyo vimesema kuwa mlipuko huo ulitokea katika eneo la Hassan Abad ambapo kuna ripoti tofauti kuhusiana na idadi ya watu waliouawa.
Swadiq Swadiqi, Msemaji wa Wizara ya Ndani ya Afghanistan amesema kuwa watu saba waliuawa katika mlipuko huo na wengine 15 kujeruhiwa. Amesema gaidi mwingine aliyekuwa na nia ya kujilipua kwa njia hiyo katika eneo hilo alinaswa na kutiwa nguvuni na polisi.
Mlipuko huo unatokea katika hali ambayo Mulla Muhammad Omar, Kiongozi wa kundi la Taliban ametoa wito hivi karibuni akiwataka wafuasi wa kundi hilo wajiepushe kutekeleza mashambulio ya kigaidi dhidi ya raia wasio na hatia. 894345
captcha