IQNA

Jumuiya ya Waislamu wa Ufaransa yalaani uvunjiwaji heshima msikiti

15:47 - November 09, 2011
Habari ID: 2219602
Jumuiya ya Waislamu wa Ufaransa RMF imetoa taarifa ikilaani vikali uvunjiwaji heshima msikiti mmoja katika mji wa Saint Amand Les Eaux kaskazini mwa nchi hiyo.
Katika taarifa hiyo jumuiya hiyo ambayo ni moja ya jumuiya muhimu za Ufaransa imeleaani vikali shambulio la watu wasiojulikana walioshambulia msikiti huo na kuandika kwenye milango na kuta zake maandishi ya chuki dhidi ya Uislamu.
Imelaani shambulio hilo lililofanyika mkesha wa kuamkia sikuu ya Idul Adh'ha na kusema kuwa Waislamu wamesikitishwa sana na vitendo vinavyoongezeka nchini humo kila siku vya kushambuliwa maeneo yao ya ibada.
Jumuiya iliyotajwa imesema katika taarifa hiyo kwamba inataraji serikali ya Paris pamoja na vyombo vya usalama vitachukua hatua za lazima kwa madhumuni ya kuwatia nguvuni na kuwahukumu wahusika wa kitendo hicho cha chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu.
Waislamu pia wamesisitiza mfungamano wao na wenzao wa Saint Amand Les Eaux na kuwaomba wawe na utulivu katika mazingira haya magumu.
Jumuiya hiyo imewataka wachukue hatua za tahadhari na kutotumbukia kwenye mtego wa wabaguzi ambao wanataka kuwachochea wajihusishe na vitendo vya ghasia na machafuko na kuzusha mvutano kati ya jamii tofauti za mji huo. 894998
captcha