IQNA

Mahatibu wa Ijumaa wa Lebanon:

Syria haitasalimu amri mbele ya maamuzi ya Arab League

16:45 - November 19, 2011
Habari ID: 2224812
Mahatibu wa Sala za Ijumaa zilizoswaliwa jana katika maeneo mbalimbali ya Lebanon wamekosoa uamuzi usiokuwa wa kimantiki wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) wa kusimamisha uanachama wa Syria na kusisitiza kuwa taifa la Syria halitasalimu amri mbele ya maamuzi hayo na litalinda matunda ya kitaifa ya nchi hiyo.
Mjini Beirut, Sayyid Ali Fadhlullah khatibu wa Msikiti wa Hassanain amesema umma wa Kiarabu na Kiislamu hii leo unapita katika kipindi hatari sana cha historia na thamani za umma zinakabiliwa na vizingiti vingi.
Sayyid Fadhlullah amesema kuwa makundi ya kigeni yanafanya njama za kutumia vibaya hali ya sasa na kuingilia mambo ya umma wa Kiislamu na Kiarabu kwa maslahi yao.
Ameashiria maamuzi yaliyochukuliwa hivi karibuni na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu Syria na kusema: "Nchi za Kiarabu zinapaswa kushirikiana katika kukabiliana na makundi ya kieneo na kimataifa yanayoingilia masuala ya ndani ya Syria ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kutetea masuala ya Waarabu hususan taifa linalokandamizwa la Palestina."
Hatibu wa Msikiti wa Hassanain mjini Beirut amesema kuwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu inawajibika kutekeleza wajibu wake ipasavyo na kufanya jitihada za kutatua matatizo ya ndani ya Syria na si kuchochea zaidi hali ya mambo. 900491
captcha