IQNA

Kituo cha Qur'ani cha wanawake chafunguliwa Qatar

16:11 - November 29, 2011
Habari ID: 2231415
Kituo cha Qur'ani Tukufu kwa jina la Ali bin Hussein as-Sada maalumu kwa wanawake, kilifunguliwa jana Jumatatu katika mji wa Shimal nchini Qatar kwa ufadhili wa Idara ya Uhubiri na Mwongozo wa Kidini ya Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa gazeti la ar-Raya linalochapishwa huko huko Qatar, Hamad bin Abdallah al-Mahna al-Mari, naibu mkuu wa idara iliyotajwa amesema kuwa kituo hicho kitakachojishughulisha na mafunzo ya kiraa na hifdhi ya Qur'ani Tukufu, kinajumuisha majengo mawili makubwa. Amesema jengo moja litatumiwa kwa masuala ya kiidara na ofisi za walimu wa Qur'ani na la pili katika kuendeshea masomo ya wanafunzi ambao watahitimu masomo yao baada ya kupitia hatua nne muhimu za masomo ya Qur'ani.
Hamad bin Abdallah al-Mahna amesema kituo hicho kimeanzishwa kwa madhumuni ya kutoa mchango katika kuhudumia Qur'ani Tukufu kwa tabaka la wanawake ambao wanaunda sehemu muhimu ya jamii ya mwanadamu.
Huku akisisitiza kwamba kituo hicho kinaandaa mazingira ya kutoa masomo ya Qur'ani kwa wanawake na mabinti wenye umri tofauti, al-Mari amesisitiza kwamba kituo hicho kina mipango madhubuti ya kutoa masomi hayo hata kwa mabinti walio na umri wa chini kabisa.
Amesisitiza kuwa mbali na kutoa masomo, kituo hicho pia kina mipango ya kuandaa mashindano ya Qur'ani na safari tofauti za masomo ili kuwapa moyo wa kufanya hima zaidi masomoni wanafunzi wa kituo hicho. 907664
captcha