Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Misri, Chama cha Uhuru na Uadilifu kimeshinda hatua hiyo ya kwanza ya uchaguzi kwa kujipatia asilimia 40 ya kura. Vyama vilivyofuata ni vya Nur kilichopata asilimia 20 ya kura, Kutlatul Misriyya asilimia 15 Hizbul Wasat asilimia 6, Alwafd asilimia 5 na Inqilab Mudawim kilichopata asilimia 3.
Abdul Muizz Ibrahim, mkuu wa tume ya uchaguzi ya Misri amesema kwamba asilimia 62 ya Wamisri walishiriki katika uchaguzi huo ambao ni wa kwanza kufanyika nchini baada ya kung'olewa madarakani dikteta Hosni Mubarak.
Uchaguzi huo ulifanyika Jumatatu na Jumanne katika mikoa tisa ya nchi hiyo. Hatua ya pili ya uchaguzi huo imepangwa kufanyika tarehe 14 na 15 za mwezi huu wa Disemba na ya tatu itafanyika tarehe 3 na 4 za mwezi Januari mwakani.
Baraza Kuu la Kijeshi la Misri limelazimika kuandaa uchaguzi huo katika hatua tatu kutokana na uhaba wa maafisa usalama wa kusimamia zoezi zima la uchaguzi kwa wakati mmoja. Kila hatua ya uchaguzi huo imepangwa kufanyika katika mikoa tisa. 909662