IQNA

Maombolezo ya Ashura yafanyika kwa mara ya kwanza nchini Misri

16:01 - December 07, 2011
Habari ID: 2234739
Maombolezo ya Ashura na kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) yamefanyika kwa mara ya kwanza nchini Misri baada ya kung'olewa madarakani utawala wa kidikteta wa Hosni Mubarak.
Maombolezo hayo hayakukamilika vizuri kutokana na mashambulio ya Masalafi wa Kiwahabi wa nchi hiyo walio na uadui mkubwa na Watu wa Nyumba ya Mtume (saw).
Kwa mujibu wa televisheni ya al-Alam, mbali na Waislamu wa madhehebu ya Shia, Masuni pia walishiriki katika maombolezo hayo ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as). Kabla ya Masalafi wa Kiwahabi kushambulia marasimu ya maombolezo hayo yaliyopangwa kufanyika katika eneo takatifu la Haram ya Ra's al-Hussein (as), waombolezaji walikuwa wameweka bendera na vitambaa vyeusi katika eneo hilo kama alama ya maombolezo, ambapo waombolezaji walikuwa wakikaribishwa katika eneo hilo na viongozi wa Mashia akiwemo Muhammad ad-Dureini, Kiongozi wa Baraza Kuu la Ahlul Bait (as) la Misri.
Akizungumza katika maombolezo hayo kabla ya kuvamiwa na Mawahabi, Ahmad Subh mmoja wa wanazuoni wa Kishia wa Misri alisema kuwa Mashia wanafuata na kutekeleza kikamilifu mafundisho ya Imam Hussein (as) ya kueneza umoja na mshikamano kati ya Waislamu.
Sheikh Ahmad Subh ameongeza kuwa mapinduzi yanayoshuhudiwa sasa katika nchi za Kiarabu yanafanyika dhidi ya Mayazidi wa zama hizi na kuzitaka taasisi za kidini za al-Azhar, Najaf na Saudi Arabia kufanya juhudi za kuwaunganisha Waislamu. 911436
captcha